CHINA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Xi Jinping afanya ziara ya kwanza Wuhan

Rais wa China Xi Jinping akiongea na wakaazi wa Beijing, Februari 10, 2020.
Rais wa China Xi Jinping akiongea na wakaazi wa Beijing, Februari 10, 2020. Xinhua via REUTERS

Rais wa China Xi Jinping amefanya ziara ya kwanza na ya kushtukiza, katika mji wa Wuhan, ambapo virusi vya ugonjwa wa Covid-19 vilianza kuripotiwa nchini China.

Matangazo ya kibiashara

Idadi ya kesi mpya za watu walioambukizwa virusi vya ugonjwa hatari wa Covid-19 inaendelea kupungua siku baada ya siku. Kwa mara ya kwanza, Rais wa China amezuru mji wa Wuhan Jumanne asubuhi, Machi 10.

Ziara hii imedhamiria kuonyesha kuwa vita dhidi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19 imeshinda nchini China.

Rais wa China amefanya ziara hiyo ya kushtukiza katika mji wa Wuhan, akiwa na malengo ya kuonyesha kuwa ugonjwa wa Covid-19 umedhibitiwa nchini China, kuwatia moyo na kuwahakikishia wakaazi wa mji huo kuwa juhudia za kupambana dhidi ya ugonjwa huo zinaendelea kuzaa matunda.

"Kwa sasa ugonjwa wa Covid-19 umedhibitiwa , hali inaweza tena kurudi kama hapo awali" , amesema rais wa China.

Mipuko wa ugonjwa wa Covid-19 ulianzia China na kuenea duniani.

Chini ya mwezi mmoja, virusi vya Corona viliripuka kuwa janga kubwa la afya na kuwaua watu karibu 500 na kuwaathiri karibu wengine 6,000. Wanasayansi wanahangaika kutafuta chanjo ya kukabiliana nacho.

Desemba 31, 2019 China ililiarifu Shirika la Afya Duniani, WHO, kuhusu visa vya maambukizi ya virusi kwenye mji wa Wuhan ulio na wakaazi milioni 11. Mzizi wa virusi hivyo haukujulikana na wataalamu wa maradhi duniani kote wakaanza kufanya kazi ili kuvibaini. Chanzo kikabainika kuwa ni soko la vyakula vya baharini katika mji huo, na kufungwa kwa haraka. Watu 40 wakaripotiwa kuambukizwa.