UGANDA-AFYA-CORONA

Abiria wanaoingia Uganda kutoka Uingereza na Marekani kuwekwa karantini

Virusi vya Covid-19 vyaendelea kuzua hofu duniani.
Virusi vya Covid-19 vyaendelea kuzua hofu duniani. REUTERS/Josiane Kouagheu

Wizara ya afya nchini Uganda imetangaza abiria wote wanaoingia nchi hiyo kutoka mataifa mengine na wamezuru mataifa ya Uingereza na Marekani katika majuma mawili yaliyopita, watapaswa kuwekwa karantini.

Matangazo ya kibiashara

Katika kipindi hicho cha kutengwa, watalazimika kuzingatia usafi na kutotangamana na watu wengine hadi wathibitishwe hawajaambukizwa.

Mapema wiki hii Wizara ya Afya nchini humo ilisema raia wa kigeni 22 waliokuwa wamewasili nchini humo kutoka katika mataifa yaliyoathiriwa na maambukizi ya Corona na kuombwa kutengwa kwa siku 14 watarudishwa katika nchi zao baada ya kukataa utaratibu huo wa serikali.

Wageni hao walikuwa wamewasili nchini humo kuhudhuria mkutano wa kibiashara kati ya Uganda na bara Ulaya ambao unaanza leo na kumalizika kesho.

Waziri wa Afya wa Uganda Ruth Aceng, pia alitangaza mataifa ambayo raia wake hawataruhusiwa nchini humo kwa sasa.

Mapema mwezi Februari wasafiri zaidi ya 100 waliwekwa karantini baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege mjini Kampala nchini Uganda wakitokea nchini China.

Raia 44 wa China ni miongoni mwa wasafiri hao waliowekwa karantini.

Mamlaka ya uwanja wa ndege nchini nchini humo ilisema uamuzi huo ulichukuliwa ili kuepusha hatari ya maambukizo ya virusi vya Covid-19 ambavyo husababisha maafa muda mfupi baada ya mtu kuambukizwa.