DRC-CORONA-AFYA

Kisa cha pili cha maambukizi ya virusi vya Covid-19 chathibitishwa DRC

Moja ya barabara wa jiji la Kinshasa. (Picha ya kumbukumbu).
Moja ya barabara wa jiji la Kinshasa. (Picha ya kumbukumbu). AFP PHOTO / PAPY MULONG

Mtu wa pili amepatikana na maambukizi ya virusi vya ugonjwa hatari wa Covid-19 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ay Congo, mamlaka nchini humo imetangaza.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano wa dharura kuhusu ugonjwa wa Covid-19 ulifanyika Alhamisi hii, Machi 12. Hatua kadhaa zimechukuliwa na viongozi, lakini hatua hizo zilizotangazwa zimeanza kukosolewa na wakaazi wa mji wa Kinshasa, wakisema kuwa hazina nguvu yoyote ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa Covid-19.

"Kesi ya pili ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19 imethibitishwa nchini DRC. Mtu ambaye amepatikana na virusi vya ugonjwa huo ni raia kutoka Cameroon. Kwa hivi sasa amelazwa katika hospitali moja jijini Kinshasa ambapo anaendelea kupata huduma mbalimbali za matibabu. Wizara ya Afya kwa mara nyingine imewahimiza raia kuzingatia kanuni za usafi ", Wizara ya Afya imeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Alhamisi Machi 12, Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilunkamba alikutana na viongozi wa afya. Mkutano ambao Waziri wa Afya, lakini pia Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Uchukuzi na Michezo walishiriki. Hataua kadhaa zilichukuliwa ili kuimarisha hatua za usafi wa mwili na haswa hatua kali kwenye mipaka.

Waziri wa Afya, Dk Eteni Longondo, amewahakikishia raia kwamba watu wapatao 109 ambao waliwasiliana na mtu wa kwanza aliyepatikana na virusi vya ugonjwa wa Covid-19, wamewekwa karantini ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

"Serikali imechukua hatua zote," Waziri wa Afya Dk Eteni Longondo amesema, na kuongeza kuwa "katika hatua hii, kuvaa mask sio lazima".