DUNIA-CORONA-AFYA

Corona yaendelea kusambaa na kusababisha vifo duniani

Virusi hivi vya Corona huleta dalili za homa kwa watu walioambukizwa, hadi kusababisha matatizo ya kupumua.
Virusi hivi vya Corona huleta dalili za homa kwa watu walioambukizwa, hadi kusababisha matatizo ya kupumua. AFP

Shirika la Afya duniani liliutangaza mlipuko wa virusi vya corona kuwa ni janga la kimataifa, huku mlipuko huo ukiendelea kusambaa katika mataifa mbalimbali duniani.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu Shirika la Afya Duninai (WHO), Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema kuwa idadi ya visa nje ya China vimeongezeka mara 13 kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita.

“Janga ni ugonjwa ambao unasambaa katika nchi nyingi kote duniani kwa wakati mmoja” , aliongeza Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Tayari nchi kadhaa duniani zimeanza kuchukua mikakati mbalimbali ya kupambana dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kuwa mipaka ya nchi hiyo itafungwa kuanzia Jumatano wiki hii kuzuia raia wa kigeni kutoka mataifa yaliyothiriwa zaidi na maambukizi ya Corona, kama njia mojawapo ya kupambana na maambukuzi hayo.

Aidha ametangaza kufungwa kwa shule zote nchini humo kwa wiki tatu kuanzia siku ya Jumatano wiki hii, wakati huu taifa likiripoti visa 61 vya maambukizi hayo.

Nchini Kenya, rais Uhuru Kenyatta ameamuru shule zote za kushinda kutwa nzima kufungwa kuanzia siku ya Jumatatu. Shule za mabweni zimepewa muda hadi Jumatano kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea nyumbani kwa sababu ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19. Vyuo vikuu na vimepewa muda hadi Ijumaa kuwapa nafasi wanafunzi wote kurejea nyumbani.

Ujerumani imeamua kufunga mipaka yake na mataifa ya Austria, Uswisi na Ufaransa kuanzia leo Jumatatu asubuhi katika hatua ya kupambana na kusambaa kwa virusi vya Corona, lakini itaendelea kuwaruhusu wasafiri wanaovuka mipaka kila siku kwa ajili ya kwenda kazini pamoja na uingizaji wa bidhaa, kulingana na magazeti mawili ya Der Spiegel na Bild yaliyoripoti.

Iran jana iliwatolea wito raia wake kuzingatia miongozo na kusalia majumbani ili kuzuia kusambaza kwa virusi vya Covid-19 wakati ikitangaza vifo vingine 113 vilivyotokana na ugonjwa huo. Idadi ya vifo iliyotolewa na wizara ya afya ya Iran imefikia watu 724 tangu ugonjwa wa Covid-19 ulipoingia nchini humo mwezi uliopita.

Nchini Morocco, maelfu ya watalii wamekwama baada ya usafiri wa ndege kati ya taifa hilo na nchi nyingine 30 duniani kusitishwa kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na virusi vya Corona.