EU-CORONA-AFYA

Coronavirus: Ulaya yajiandaa kuchukua hatua za kupambana dhidi ya Covid-19

Askari wakipiga doria kwenye mitaa ya Madrid, Machi 16, 2020, baada ya kutangaza hali ya hatari kutokana na virusi vya ugonjwa hatari wa Covid-19.
Askari wakipiga doria kwenye mitaa ya Madrid, Machi 16, 2020, baada ya kutangaza hali ya hatari kutokana na virusi vya ugonjwa hatari wa Covid-19. REUTERS/Juan Medina

Umoja wa Ulaya unajiandaa kutokomeza kabisa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 ambavyo vimeua zaidi ya watu 6,500 duniani, hasa barani Ulaya ambapo wimbi la wagonjwa limesababisha nchi kadhaa kuwazuia raia wao na kufunga mipaka yao.

Matangazo ya kibiashara

Upande wa Ulaya, Paris imetangaza kwamba hatua kali kwenye mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya "zitakamilika na kutangazwa katika saa zijazo ", baada ya mazungumzo kati ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na rais wa Tume ya umoja huo Ursula von der Leyen.

Bw. Macron, ambaye anatarajia kulihutubia taifa leo Jumatatu jioni, ametoa wito "kuongeza mikakati madhubuti katika ngazi ya Ulaya na kuchukua hatua haraka na kwa makubaliano, hasa kuhusu mipaka ya Umoja wa Ulaya", huku akilaani "hatua zilizochukuliwa na nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya bila makubaliano yoyote kuhusu mipaka".

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte, ambaye nchi yake imeathirika zaidi na ugonjwa huo barani Ulaya, ametoa wito wa "Ulaya kushirikiana kwa karibu" katika nyanja ya afya na uchumi.

Janga hili la virusi vya Corona linaendelea kuutikisa ulimwengu, huku nchi mbali mbali zikiongeza juhudi na hatua za kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo hatari kabisa.

Mawaziri wa Fedha wa Umoja wa Ulaya wanapanga kufikia makubaliano ya pamoja ya kiuchumi katika kukabiliana na janga hili ambalo, tayari imetabiriwa na Umoja wa Ulaya huenda likasababisha zahma kubwa ya kiuchumi katika umoja huo.

Mawaziri hao watajadiliana kwa njia ya vidio kuhusu jinsi ya kupunguza athari za kuenea kwa virusi vya Corona ambavyo tayari vimeshasababisha nchi nyingi za Ulaya kuchukua hatua ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.