RWANDA-CORONA-AFYA

Rwanda yathibitisha visa vinne vipya vya maambukizi ya Covid-19

Manispaa ya mji wa Kigali, Rwanda.
Manispaa ya mji wa Kigali, Rwanda. RFI/Laure Broulard

Serikali ya Rwanda imethibitisha visa vingine vinne vya maambukizi ya Covid-19 (Corona) na kufikisha idadi ya watu walioambukizwa kufikia watano, hali ambayo raia wanaendelea kuwa na hofu.

Matangazo ya kibiashara

Wagonjwa wote waliwasili nchini Rwanda kutoka mataifa yaliyoathiriwa wakati huu serikali ya nchi hiyo ikitangaza hatua zaidi dhidi ya maambukizi hayo ambayo sasa yamefika katika eneo la Afrika Mashariki.

Rwanda ilithibitisha kisa chake cha kwanza cha virusi vya Corona (COVID-19) Jumamosi ya wiki hii iliyopita. Mgonjwa huyo ni raia wa India aliyewasili Rwanda Machi 8 kutoka Mumbai, India, kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya afya.

Raia huyo hakuwa na dalili zozote za virusi vya Corona wakati aliwasili nchini Rwanda na alijipeleka mwenyewe kwenye kituo cha afya Machi 13, ambapo alifanyiwa vipimo mara moja.

Hata hivyo kupitia mahojiano na kituo cha redio cha taifa cha Radio Rwanda, Waziri wa Afya wa Rwanda Dkt Ngamije Daniel, alisema kwamba nchi yake iko tayari kupambana na virusi hivyo.

Kupitia ujumbe wake katika mtandao wa Twitter, Rais Paul Kagame amewatakia wagonjwa wote afueni ya haraka na kumshukuru Dr Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkuu wa Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa (WHO), na idara yote kwa ujumla kwa uongozi wao wakati huu wa majaribu na kuwaombea wahudumu wa afya kuendelea kuwa imara wanapokuwa mstari wa mbele kukabiliana na janga hili.

Raia wametakiwa kutohudhuria mikusanyiko ya umma na kuarifu mamlaka iwapo watashuhudia tukio wanalolishuku kupiga simu kupitia nambari 114.

Wakati huo huo shirika la ndege la Rwanda, Rwandair, limetangaza kusitisha safari zake za ndege kwa muda kwenda nchini India kwa sababu ya mlipuko wa Corona hadi Aprili 30, 2020.