TANZANIA-CORONA-AFYA

Coronavirus / Tanzania: Shule zote zafungwa kwa siku 30

Dar es-Salaam, mji wenye watu wengi nchini Tanzania, ambapo wengi wana hofu ya kupata ugonjwa wa Covid-19 kwa urahisi kutokana nawingi wa watu..
Dar es-Salaam, mji wenye watu wengi nchini Tanzania, ambapo wengi wana hofu ya kupata ugonjwa wa Covid-19 kwa urahisi kutokana nawingi wa watu.. Wikimédia/Muhammad Mahdi Karim

Serikali ya Tanzania kupitia waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza kufunga shule zote, ikiwa ni moja ya hatua ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19 nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

“Serikali ya Tanzania imefunga shule zote kwa siku 30 kuanzia leo Jumanne Machi 17, 2020, ” amesema Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Katika hatua nyingine ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa huo hatari, serikali ya Tanzania imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu, hususan michuano mbalimbali ya soka na michezo mingine inayokutanisha watu mbalimbali katika maeneo mbalimbali na shuleni (UMITASHUMTA na UMISETA), michezo ya mashirika ya umma pamoja na mikusanyiko yote ya watu wengi.

Hatua hizi zinakuja siku moja tu baada ya mtu wa kwanza, raia wa Tanzania, kubainika kuwa na virusi vya Ugonjwa wa Covid-19.

Mgonjwa aliyetangazwa ni mwanamke wa miaka 46 raia wa Tanzania, ambaye aliwasili kutoka Ubelgiji kwa ndege ya shirika la Rwanda.

Jumatatu wiki hii Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu alisema mgonjwa huyo aliwasili na ndege ya shirika la Rwanda akitokea nchini Ubelgiji, moja ya taifa ambalo na lenyewe limeathirika pakubwa na virusi hivyo.

Jana Jumatatu rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, alitangaza kusitishwa kwa mbio maarufu za mwenge wa uhuru, ambapo aliagiza fedha zote zilizokuwa zimepangwa kutumika, zielekezwe katika vita dhidi ya Corona.

Nchi mbalimbali zimeendelea kuchukuwa hatua katika hali ya kuzuia kusambaa kwa virisi vya ugonjwa hatari wa Covid-19, ambao Shirika la afya Dunia, WHO, liliutaja kuwa ni janga la kimataifa.