AFRIKA-CORONA-AFYA

Nchi za Afrika zaendelea kukubiliana na janga la Corona

Rais wa Côte d'Ivoire Alassane Ouattara wakati wa kikao cha Baraza la usalama la kitaifa kuhusu janga la Covid-19, Machi 16, 2020.
Rais wa Côte d'Ivoire Alassane Ouattara wakati wa kikao cha Baraza la usalama la kitaifa kuhusu janga la Covid-19, Machi 16, 2020. SIA KAMBOU / AFP

Nchi kadhaa za Afrika zimetangaza makataa zaidi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Covid-19.

Matangazo ya kibiashara

Ugonjwa wa Covid-19 mpaka sasa umesababusha vifo vya watu 7,000 duniani, hasa barani Ulaya ambapo idadi ya vifo inaendelea kuongezeka kwa mujibu wa shirika la Habari la AFP.

Bara la Afrika ambalo, kwa muda mrefu limekuwa halijakumbwa na uginjwa huo, ambao umekuwa janga la kimataifa, leo linaendelea kukabiliana na visa vya kwanza vya ugonjwa huo katika nchi mbalimbali. Kesi za maambukizi ambazo, sio nyingi, zimekuwa zikishughulikiwa, lakini inaonekana kuwa huenda idadi ya visa vya maambukizi ikaongezeka katika siku za hivi karibuni. Hatua zilizotangazwa katika saa za hivi karibuni ikilinganishwa na zile zilizokuwa zikitarajiwa na raia, zimezua hofu katika nchi kadhaa.

■ Mamlaka nchini Côte d'Ivoire imetangaza hatua kadhaa za kupambana na kusambaa kwa ugonjwa huo. Nchi hii sasa ina wagonjwa sita wa Covid-16 waliothibitishwa, afisa mwandamizi katika ofisi ya rais alisema Jumatatu usiku wiki hii. "Mgonjwa wa kwanza amepona na wagonjwa wengine wanaendelea vizuri", pia amesema Patrick Achi baada ya kikao cha Baraza la usalama la kitaifa kilichofanyika Jumatatu jioni. Wakati huo huo hatua kumi na tatu zimechukuliwa: Mikusanyiko ya watu zaidi ya hamsini imepigwa marufuku, vilabu vya usiku vimefungwa, majumba ya sinema na kumbi za starehe na muziki zimefungwa, matukio ya michezo na kitamaduni imesitishwa kwa siku 15.

Wasafiri, ambao sio raia wa taifa hilo kutoka nchi zilizo na kesi zaidi ya 100 wamepigwa marufuku kuingia nchini humo kwa angalau siku 15. Raia wa nchi hiyo wanaorudi nchini pamoja na wakaazi wasiokuwa raia wa nchi hiyo watawekwa karantini kwa siku 14 watakapo wasili nchini humo.

Hatua nyingine ni kuwa shule zote zitafungwa kuanzia leo Jumanne kwa muda wa mwezi mmoja

■ Senegal imesitisha safari za anga kutoka au kwenda katika baadhi ya nchizilizoathirika na ugonjwa wa Covid-19, hususan Ufaransa, Uhispania, Ubelgiji, Ureno, Algeria na Tunisia.

Hatua hizo zilizotangawa Jumatatu na Waziri wa Utalii na Uchukuzi wa anga zitaanza kutumika Jumatano (saa 11.59 usiku), kwa muda wa siku 30.

Hatua hizi mpya zinakwenda sambamba na zile zilizochukuliwa awali na rais Macky Sall Jumamosi wiki iliyopita: mikusanyiko ya hadhara imepigwa marufuku, shule na vyuo vikuu vimefungwa. Kulingana na taarifa ya hivi karibuni kutoka Wizara ya Afya, Senegal ina wagonjwa 27 wa Covid-19, hata hivyo wawili wamepona.

■ Chad kwa sasa imefunga mipaka yake kwa safari za kimataifa kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona. Hatua ambayo itaanza kutumika Alhamisi wiki hii. Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu wiki hii, serikali ya Chad inasema hakuna kesi za Covid-19 lakini inatoa wito kwa wakaazi kuheshimu na kufuata hatua kadhaa za kiusalama.

Mikusanyiko ya watu zaidi ya hamsini imepigwa marufuku nchini Chad.

Hatua kama hizo zimechukuliwa katika nchi nyingi barani Afrika, ikiwa ni pamoja na Rwanda, Kenya na Ethiopia.