AFRIKA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Nchi za Afrika zaendelea kukabiliana na kusambaa kwa virusi

Wafanyakazi katika sekta ya usafiri wakiosha mikono yao kabla ya kuingia katika kituo cha magari cha Nairobi, Kenya, Machi 17, 2020.
Wafanyakazi katika sekta ya usafiri wakiosha mikono yao kabla ya kuingia katika kituo cha magari cha Nairobi, Kenya, Machi 17, 2020. REUTERS/Baz Ratner

Afrika ndio bara pekee kati ya mabara matano ambayo ilichelewa kukumbwa na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona, lakini idadi ya visa vya maambukizi imeongezeka haraka.

Matangazo ya kibiashara

Barani Afrika watu 462 ndio wameripotiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19 hadi Jumanne, Machi 17 kabla ya usiku wa manane, ikiwa ni pamoja na kesi 166 nchini Misri.

Mamlaka katika nchi mbalimbali barani Afrika zimeendelea kuhamasisha raia kuhusu ugonjwa huo.

Hatua zilizochukuliwa ni sawa na zile zilizochukuliwa katika nchi zilizoathirika.

■ Nchini Cameroon, serikali imetangaza hatua kadhaa za kujaribu kupunguza kuenea kwa virusi vya Covid-19 nchini. Hatua ambazo zinaanza kutumika Jumatano hii Machi 18. Katika taarifa iliyosomwa katika runinga ya taifa, Waziri Mkuu wa Cameroon, Joseph Dion Ngute, alitangaza hatua ambazo zinaanza kutumika Jumatano wiki hii katika kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Covid-19:

- mipaka ya ardhini, angani na baharini imefungwa

- Zoezi la kutoa visa ya kuingia nchini Cameroon limesitishwa

- shule zote, kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu, katika sekta ya umma na binafsi hatimaye zimefungwa

- Mikusanyiko ya watu zaidi ya 50 imepigwa marufuku

- Sehemu za starehe, baa na mikahawa kutozidisha saa 12 jioni

■ Licha ya kuwa ugonjwa wa Covid-19 haujaripotiwa nchini Niger, serikali imechukuwa hatua kumi muhimu katika hali ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa huo.

■ Pia ugonjwa wa Covid-19 haujaripotiwa nchini Mali. Lakini serikali ya Bamako imetoa nasaha kwa raia wake, na Baraza Kuu la Ulinzi lilikutana Jumanne wiki hii chini ya uongozi wa rais Ibrahim Boubacar Keita, kikao ambacho wanasayansi, Waziri Mkuu na mawaziri ikiwa ni pamoja na wale wa Ulinzi na Afya walishiriki. Hatua kadhaa zimechukuliwa kwa kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo:

- safari zote kutoka nchi zilizoathiriwa zimesitishwa (ispokuwa tu ndege za mizigo)

- shule za umma, za kibinafsi na zile zinazomolikiwa na dini, pamoja na madrasa zimefungwa kwa muda wa wiki tatu.

- mikusanyiko ya watu zaidi ya hamsini imepigwa marufuku. Hata hivyo serikali haijabaini iwapo kampeni ya uchaguzi wa wabunge imesitishwa au la.

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita (IBK) ameagiza Faranga za CFA bilioni 6 zielekezwe katika kukabiliana na hali hiyo.

■ Jumanne jioni Machi 17, Waziri wa Afya wa Sudan alisema kwamba hapajakuwa na kesi mpya tangu kufariki dunia kwa mtu mwenye umri wa miaka 50 aliyeambukizwa virusi vya Covid-19 wiki iliyopita. Hata hivyo watu 54 wako chini ya uangalizi.

Wakati huo huo serikali imechukuwa hatua kadhaa za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa huo.