KENYA-UTALII-CORONA-AFYA

Coronavirus: Sekta ya utalii Kenya yaathirika

Fort-Jesus, moja ya makavazi jijini Mombasa.
Fort-Jesus, moja ya makavazi jijini Mombasa. Wikipedia/Domaine public

Sekta ya utalii nchini Kenya imeathirika pakubwa kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 uliosababisha serikali nyingi kuzuia raia wake kusafiri nje ya nchi zao.

Matangazo ya kibiashara

Mohamed kale, mhudumu wa kuwatembeza watalii katika maeneo tofauti ambaye amekutana na mwandishi wetu ykatika eneo la makavazi ya Fort Jesus, mjini Mombasa, amesema mlipuko wa ugonjwa huo wa corona umesababisha madhara makubwa kwa sekta ya utalii.

“Ni mwezi mzima sasa hatuna kazi, tangu kuibuka kwa ugonjwa huo. Tunakuja hapa, lakini hakuna shughuli yoyote tunayofanya, muda ukifika kila mmoja anarudi nyumbani kulala. Unajua sisi wakaazi wa Pwani tunategemea sana sekta ya utalii, ikiwa sekta hii hifanyi kazi, tutafanya nini? “

Sam Ikwaye, mkurugenzi mtendaji katika muungano wa wamiliki wa hoteli za kitalii nchini Kenya, amesema kwa sasa hoteli nyingi zimerekodi idadi ya chini ya watalii kufuatia marufuku ya kusafiri kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

“Kwa hivyo watu hawawezi kusafiri tena, inamaanisha hatuwezi kuwa na watu wanaohitaji kuja katika hoteli zetu, na hivyo imechangia pakubwa idadi ya watalii wanaokuja hadi asilimia 50, “ amesema Sam Ikwaye.

Margret Olang' mshika dau wa utalii eneo la pwani, amepongeza hatua ya mataifa yaliyozuia safari za ndege kuja nchini Kenya.

“Itakuwa hasara kwetu na tusifikirie biashara sana dhidi ya maisha yetu. Mimi naomba ikiwa ugonjwa huo wa Corona utakuwa bado haujapata dawa au kinga, marufuku hiyo ya kusafiri iendelee lkwa nchi zote.

Rfi kiswahili imezungumza na Joe Ave, raia wa Italia, ambaye ameishi nchini Kenya kwa muda wa mwezi mmoja sasa, ambaye anabaini kwamba yuko na marafiki zake ambao wanatamani sana kuja Kenya, lakini hawawezi kuja kwa sababu safari za ndege zilisitishwa.

Kwa Sasa mataifa ya Afrika Mashariki yametangaza mikakati ya kukabili maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.