TANZANIA-CORONA-AFYA

Tanzania yashuhudia ongezeko la visa vya maambukizi ya Corona

Moja ya maeneo yanayotembelewa na watu wengi Dar es Salaam.
Moja ya maeneo yanayotembelewa na watu wengi Dar es Salaam. Bruno Minas / RFI

Tanzania inaendelea kukabiliwa na ongezeko la visa vya maambukizi ya ugonjwa hatari wa Covid-19. Baada ya mtu wa kwanza, raia wa Tanzania kubainika na virusi vya ugonjwa huo, visa vingine vipya viwili vimeripotiwa kisiwani Zanzibar na Dar es Salaam.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya hatua kadhaa za kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo kuchukuliwa, visa vya maambukizi nchini Tanzania vinaendelea kuongezeka. Raia wawili wa kigeni wapepatikana na virusi vya ugonjwa wa Covid-19, ametangaza Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa, kwa mujibu wa gazeti la Citizen Tanzania.

Taarifa hiyo inakuja siku moja baada ya nchi hiyo kutangaza kufunga shule zote za awali hadi kidato cha sita nchi nzima pamoja na kuzuia mikusanyiko mikubwa ya watu kutokana na hofu ya kuenea kwa virusi vya Corona.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Jumanne wiuki hii, Kassim Majaliwa, ametangaza kusitishwa kwa michezo yote ikiwemo ligi kuu ya soka nchini humo ikiwemo michezo ya shule za Sekondari na msingi kwa muda wa siku 30.

Waziri mkuu pia ameagiza mamlaka za afya na vyombo vya ulinzi kuimarisha usalama kwenye maeneo ya mipaka ikiwa ni pamoja na kuwapima wageni wanaoingia nchini humo.