UINGEREZA-CORONA-AFYA

Ugonjwa wa Corona wazua sintofahamu katika shule za Uingereza

Uingereza yaendelea kuathirika na ugonjwa wa Corona.
Uingereza yaendelea kuathirika na ugonjwa wa Corona. RFI/Cécile Pompeani

Wakati serikali ya Uingereza ikiendelea kukataa kufunga shule licha ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona kuendelea kuiathiri nchi hiyo, baadhi ya shule zimeanza kufunga milango kwa kukosa wafanyakazi au wanafunzi walio tayari kwenda shuleni.

Matangazo ya kibiashara

Geoff Barton, katibu mkuu wa Chama cha viongozi wa shule, ASCL (Association of School and College Leaders), amesema kwamba itakuwa vigumu kwa wakuu wa shule kuendelea na shughuli za shule baada ya wiki hii.

"Wakuu wengine wenye uzoefu sana wananipigia simu wakisema kwamba hawataweza kuendelea na shughuli za shule," Geoff Barton ameliambia shirika la utangazaji la BBC. "Mmoja aliniambia kuwa ana wafanyakazi 17 ambao wako katika likizo kutokana na ugonjwa. Na nadhani kesi kama hizo zitandelea kutokea nchini kote, " Geoff Barton ameongeza.

Akihojiwa na kamati ya bunge Jumanne wiki hii, mshauri mkuu wa kisayansi, daktari Patrick Vallance alisema kwamba kufungwa kwa shule hizo ni jambo muhimu lakini bado uamuzi haujachuliwa.

Wazazi wengi wamekataa kupeleka watoto wao shuleni, wakifuata nyayo za nchi zingine nyingi ambazo shule zimefungwa ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Covid-19.