EU-CORONA-AFYA

Umoja wa Ulaya waweka mikakati ya kupambana na maambukizi ya Corona

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameonya kuhusu kufungwa kwa mipaka, hatua iliyochukuliwa na nchi kadhaa za umoja huo kupambana na janga la Corona huko Brussels, Machi 13, 2020.
Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameonya kuhusu kufungwa kwa mipaka, hatua iliyochukuliwa na nchi kadhaa za umoja huo kupambana na janga la Corona huko Brussels, Machi 13, 2020. REUTERS/Johanna Geron/File Photo

Tume ya Umoja wa Ulaya inapanga kupiga marufuku safari zisizo za lazima katika eneo la Schengen, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya kupambana na maambukizi ya Corona ambayo yameonekana kuongezeka katika bara hilo.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Tume hiyo Ursula von der Leyen amesema kuwa atawaomba viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya kutekeleza hatua hii ambayo amesema itasaidia sana kupunguza maambukizi ya virusi hivyo.

Masharti haya yatatekelezwa kwa muda wa siku 30 zijazo na pamoja na wananchi kutoka mataifa haya, marufuku haya yatawaathiri pia wananchi wa nchi ya Uingereza ambayo ilijiondoa kwenye Umoja huo.

Mbali na Umoja wa Ulaya, mataifa mbalilbali yamechukua hatua, yakiongozwa na Ufaransa ambayo kuanzia siku ya Jumanne, imetoa wito kwa raia wake kuepuka safari zisizo za lazima kwa siku 15 huku mipaka na nchi jirani ikifungwa kwa siku 30.

Shirika la afya duniani WHO linasema kwa sasa bara la Ulaya ndio lililoathirika zaidi na maambukizi haya, huku mataifa ya Italia na Uhispania yakifunga shughuli zote.