CONGO-UFARANSA-CORONA-AFYA-MUZIKI

Aurlus Mabélé, mfalme wa soukouss, afariki dunia kwa Corona

Moja ya kazi nzuri alizozifanya Aurlus Mabélé
Moja ya kazi nzuri alizozifanya Aurlus Mabélé Aurlus Mabélé

Mwanamuziki nguli, Aurlus Mabélé, mfalme wa soukouss, kutoka Congo-Brazzaville hayupo tena katika dunia hii tangu Alhamisi wiki hii, baada ya kuaga dunia jijini Paris, nchini Ufaransa.

Matangazo ya kibiashara

Binti yake Liza Monet ametoa taarifa hiyo kwenye vyombo vya habari vya kijamii. Mwanamuziki huyo nguli alifariki dunia baada ya kuamukizwa virusi vya ugonjwa hatari wa Covid-19.

Aurlus Mabélé, ambaye alizaliwa katika kitongoji cha Poto-Poto, jijini Brazzavile, alifariki dunia kwa Corona, binti yake ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kwa miaka kadhaa, Aurlus Mabélé alikuwa amedhoofika kiafya. Alikuwa anasumbuliwa na kiharusi.

Aurlus Mabélé alikuwa na umri wa miaka 67. Alikuwa mwanamuziki mashuhuri nchini Congo, ambaye alijulikana kwa jina la utani la mfalme wa kucheza na "kuvaa".

Tazama moja ya nyimbo zake zilizopendwa "Loketo"

Aurlus Mabélé aliongozana na mwanamuziki maarufu mwingine Diblo Dibala katika kazi yake hiyo ya kimuziki. Aurlus Mabélé, ambaye jina lake halisi ni Aurélien Miatsonama, alikuwa ameanzisha kikundi cha Loketo miaka ya 80. Wakati huo, alikuwa akiimba mara nyingi huko Martinique, Guadeloupe, Guyana na Reunion kwa usaidizi mkubwa wa Michel Nicole, ambaye aliandaa safari zake.

"Kazi yake ilipendwa sana kote ulimwenguni na hasa barani Afrika," anakumbuka Claudy Siar, mtangazaji wa RFI. "Alikuwa kaka mkubwa kwetu na katika kipindi hiki cha kusalia nyumbani hatutaweza kutoa heshima za mwisho kwake," ameongeza Claudy Siar.

Nyimbo zake za “Loketo, Femme ivoirienne , Vacances aux Antilles”, zitaendelea kukumbukwa.