RWANDA-UCHUMI-CORONA-AFYA

Rwanda yachukua hatua za kiuchumi kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19

Hospitali ya Ndera nchini Rwanda.
Hospitali ya Ndera nchini Rwanda. (RFI)

Rwanda imethibitisha kesi 11 za maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa Covid-19 nchini humo. Tayari, bei ya vyakula na bidha muhimu zimeendelea kuongezeka kwenye masoko mbalimbali, na sekta ya utalii imeathirika pakubwa.

Matangazo ya kibiashara

Katika kukabiliana na hali hiyo, mamlaka ya nchi hiyo imetangaza hatua kadhaa kukabiliana na kupanda kwa bei kiholela.

Benki Kuu ya Rwanda imetangaza kupunguza masharti ya ulipaji wa mikopo ya benki kwa kampuni na watu walioathirika na ugonjwa wa Covid-19.

Karibu Euro milioni 50 pia zimetolewa kwa benki za biashara, ambazo zitahitaji ukwasi zaidi. Ili kuzuia maambukizi ya virusi kupitia biashara ya fedha (kutoa na kupokea fedha), mamlaka pia imesitisha ada ambayo ilikuwa ikitozwa kwa kutoa fedha kupitia mfumo wa kidijitali.

Hatua hizo zinalenga kupunguza athari za Covid-19 kwenye uchumi wa Rwanda. Mojawapo ya sekta zilizoathiriwa zaidi ni sekta ya utalii. Angalau matukio 20 yaliyokuwa yamepangwa kufanyika mwezi Machi na Aprili yamesogezwa mbele, kwa hali hiyo Rwanda itapoteza euro milioni 7, kulingana na Ofisi ya kukusanya mapato ya Rwanda.

Wakati huo huo bei imeendelea kupanda kwenye masoko mbalimbali nchini humo, licha ya agizo kutoka Wizara ya Biashara kupanga kiwango cha juu cha bei ya mchele, sukari, au hata unga wa mahindi.

Hata hivyo, mamlaka ya serikali imeazimia kukomesha hali hiyo. Siku ya Alhamisi, Wizara ya Biashara ilitangaza kuwa itaendelea kufanya ukaguzi, na baadhi ya wafanyabiashara wamelazimika kufunga duka zao kwa muda, au kulipa faini.