SENEGAL-COTE D'IVOIRE-CORONA-AFYA

Coronavirus: Senegal na Cote d'Ivoire zatangaza hali ya dharura

Maafisa wa afya na usafi nchini Senegal wanajiandaa kupulizia dawa kwenye mitaa ya sokoni huko Dakar katika hali ya kupambana dhidi ya kuenea kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, Machi 22, 2020.
Maafisa wa afya na usafi nchini Senegal wanajiandaa kupulizia dawa kwenye mitaa ya sokoni huko Dakar katika hali ya kupambana dhidi ya kuenea kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, Machi 22, 2020. REUTERS/Zohra Bensemra

Marais wa Senegal Macky Sall na wa cote d'Ivoire Alassane Ouattara wametangaza hali ya dharura katika nchi zao. Nchi hizi mbili zimetangaza sheria ya kutotoka nje usiku, na raia wametakiwa kusalia nyumbani.

Matangazo ya kibiashara

Senegal na Cote d'Ivoire pia zimepiga marufuku mikusanyiko, kumbi za starehe na muziki zimefungwa.

Hatua zote hizo zimechukuliwa katika hali ya kuzuia kuenea kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa Covid-19 (Corona).

Rais wa Senegal Macky Sall alitangaza hali ya dharura katika nchi nzima kuanzia Jumatatu jioni, Machi 23, katika hali ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo. Sheria ya kutotoka nje usiku inaanza kutmika kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi.

Katika hotuba yake kwa taifa, rais wa Senegal amepiga marufuku mikusanyiko na safari ambazo si muhimu ndani na nje ya nchi, huku akipiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote ile, maandamano na kufunga maeneo wanakokusanyika watu wengi.

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa Wizara ya Afya, Jumatatu hii alasiri, visa vipya 12 vya maamukizi vimeripotiwa. Hadi leo, Senegal imerekodi visa 71 vya maambukizi ambavyo vinashughulikiwa, watu 8 wamepona na hakuna mtu yeyote amlbaye amefariki dunia kutokana na virusi hivyo nchini humo.

Nchini Cote d'Ivoire hali ya dharura imetangawa. Nchi hii inaripoti visa 25 vya maambukizi ya virusi vya Covid-19, na hakuna kifo chocote ambacho kimetokea kuhusiana na ugonjwa huo.

Hata hivyo hatua nane zimechukuliwa kukabiliana na kuenea kwa virusi vya ugonjwa hatari wa Covid-19 nchini Cote d'Ivoire.