Coronavirus: Bunge la Seneti la Marekani lapitisha mpango wa kuimarisha uchumi
Baraza la Seneti la Marekani limepitisha kwa kauli moja muswada unaoruhusu kutolewa kwa Dola Trilioni 2 kusaidia kuimarisha hali ya kiuchumi ambayo imeathiriwa na maambukizi ya virusi vinavyo sababisha ugonjwa hatari wa Covid-19 (Corona).
Imechapishwa:
Kwa mujibu wa wasaidizi wa Donald Trump, muswada huyo umeungwa mkono na kupitishwa na maseneta kutoka pande mbili katika Baraza la Seneti, Democrat na Republican, kwa kura 96 za wajumbe wote walioshiriki kikao hicho.
Muswada huo unatarajiwa tena kupitishwa na Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na wabunge kutoka chama cha Democratic, katika kikao kilichopangwa kufanyika Ijumaa kabla ya kutiliwa saini na rais Donald Trump.
"Ninashukuru Baraza la Seneti kuidhinisha mpango huu muhimu na kuurejesha kwangu bila kuchelewa ili uweze kutiliwa saini. Ukinifikia, basi sintochelewa kutia saini," Donald Trump alisema mapema Jumatano kwenye mkutano na waandishi wa habari.
"Tunahitaji kupata pesa hizi kuzitumia katika uchumi wa Marekani na kuzituma kwa wafanyakazi wa Marekani," amesema Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, ambaye aliongoza mazungumzo na bunge la Congress.
Hatua hizo ni pamoja na kutuma misaada ya moja kwa moja kwa Wamarekani, hadi dola 1,200 kwa mtu mzima na dola 500 kwa kila mtoto, kwa familia zinazopata chini ya dola 150,000 kwa mwaka.