DRC-CORONA-AFYA

DRC: Wakazi wa mji wa Kinshasa marufuku kutoka nje kwa muda wa wiki tatu

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefunga mji wa Kinshasa kuzuia maambukizi katika miji mingine, hatua ambayo itaanza kutumika rasmi Jumamosi Machi 28, 2020 kwa muda wa wiki tatu.

Eneo linalotembelewa na watu wengi jijini Kinshasa, Agosti 16, 2019.
Eneo linalotembelewa na watu wengi jijini Kinshasa, Agosti 16, 2019. Photo by Ute Grabowsky/Photothek via Getty Images
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo ulitolewa Alhamisi wiki hii na Gavana wa mkoa wa Kinshasa, Gentiny Ngobila.

Mkoa wa Kinshasa ni kitovu cha ugonjwa wa Covid-19 ambao tayari umesababisha vifo vya watu wanne kati ya wagonjwa 54 walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

DRC imethibitisha kuwaweka watu 2,000 karantini ambao wamehusiana na wagonjwa hao wa Covid-19.

Mmoja kati ya wagonjwa hao ni kutoka Kaskazini mwa Mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

"Kaeni nyumbani na mtatoka nje wakati ikihitajika kabisa. Hatua hiyo imewashtua wakazi wa mji wa Kinshasa.

Raia wameonekana wakilalamikia hatua hiyo ambayo serikali imeichukua kutokana na hali ya maisha ya wengi wanategemea kipato cha dola moja au chini ya hapo.

Hata hivyo Gavana Gentiny Ngobila amebaini kwamba hali hiyo inatia wasiwasi na ameamua "kufunga mji wa Kinshasa kwa muda wa wiki tatu, hatua ambayo itaanza kutekelezwa Jumamosi, Machi 28.

"Maafisa wa utawala wa umma pekee pamoja na wafanyakazi katika sekta ya afya ndio wataruhusiwa kwenda kazini, " amesema Gavana Gentiny Ngobila.

Wakati huo huo serikali ya DRC imewaonya wafanyabiashara kutopandisha gharama ya vitu wakati huu ambao hali si nzuri.