ULAYA-MAREKANi-AFRIKA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Ulaya yaathirika zaidi, Trump asema yuko makini

Raia wa Urusi na Nigeria wamejiunga na raia zaidi ya bilioni tatu duniani wanaoendelea kukaa nyumbani kwa matumaini ya kupambana dhidi ya kuenea kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa Covid-19.

New York, Machi 29, 2020: Mtaa wa Madison Avenue uko tupu kwa sababu ya janga la Covid-19 ambalo limeathiri mji huo.
New York, Machi 29, 2020: Mtaa wa Madison Avenue uko tupu kwa sababu ya janga la Covid-19 ambalo limeathiri mji huo. REUTERS/Jeenah Moon
Matangazo ya kibiashara

Ugonjwa wa Covid-19 (Corona) umeua zaidi ya watu 33,000, huku ukiiathiri zaidi Ulaya na hasa Uhispania na Italia, na kumkatisha tamaa Donald Trump ambaye alitarajia kupunguza hatua alizochukua dhidi ya ugonjwa huo haraka iwezekanavyo.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema masharti ya kuzuia maambukizi ya Corona yataendelea kutekelezwa hadi mwisho wa mwezi wa Aprili na sio wakati wa Sikuku ya Pasaka, kama ambavyo alikuwa ameahidi hapo awali.

Trump ametoa kauli hii wakati huu, idadi ya vifo katika jimbo la New York ikiongezeka na kufikia zaidi ya 2,400, huku wengine 140,000 wakiambukizwa, takwimu ambazo rais Trump amesema kuna uwezekano mkuwa wa nchi hiyo kushuhudia maafa zaidi.

Nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo wa Covid-9, Italia na Uhispania, zinaamani hatimaye kukaribia kiwango cha juu cha janga hilo. Lakini nchini marekani, ambapo kunaripotiwa karibu visa 140,000 vya maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa huo, Rais Donald Trump amebaini kwamba nchi hiyo inatarajia kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha ugonjwa huo "labda" ndani ya wiki mbili zijazo.

Mshauri wake kuhusu janga hilo, Dk. Anthony Fauci ametoa ripoti ya kutisha, akikadiria kuwa virusi vinavyo sababisha ugonjwa wa Covid-19 vitasababisha vifo vya watu "kati ya 100,000 na 200,000" nchini Marekani.

Kwa sasa Marekani inakadiria kuwa watu karibu 2,400 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa Covid-19.

Katika mji mkuu wa Urusi, Moscow, tangu Machi 8 wale ambao hawaheshimu hatua za kukaa nyumbani wanatumikia kifungo cha miaka mitano. Meya mji huo Sergei Sobianin ameamuru wakazi wote wa mji wa Moscow kubaki nyumbani.

Wakazi milioni 12.5 wataruhusiwa kuondoka katika nyumba zao kwenda kufanya kazi, ikiwa ni lazima, kwa dharura za matibabu, kwa kupata chakula au kwenda kwenye duka za dawa.Wanaweza kwenda kutupa taka na kuwatembeza mbwa wao, lakini tu kati ya mita 100 ya nyumba zao.

Serikali ya mji wa Lagos, wenye wakazi milioni 20 na ile ya Abuja, mji mkuu wa Nigeria, pia wametangaza rufuku kwa raia wao kutoka nje.

Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika na (wakazi milioni 200) ilitangaza Jumapili jioni visa 97 vya maambukizi ya virusi vya Corona, lakini idadi hiyo inaweza kupindukia haraka, alionya Waziri wa Habari Lai Mohammed, siku ya Alhamisi.