KENYA-CORONA-AFYA

Kenya yaendelea kuathirika kutokana na ugonjwa wa Covid-19

Watu wanne zaidi wameambukizwa virusi vya Corona nchini Kenya na kufikisha idadi ya wagonjwa kufikia 42, wakati huu serikali nchini humo ikiendelea kutekeleza amri ya watu kutotoka nje, ambayo imeathiri shughuli za biashara hasa, katika Pwani ya nchi hiyo.

Mfanyakazi wa Wizara ya Afya ya Kenya akipulizia dawa kwenye katika maezneo mbalimbali ya soko ya jiji la Nairobi, Machi 21, 2020.
Mfanyakazi wa Wizara ya Afya ya Kenya akipulizia dawa kwenye katika maezneo mbalimbali ya soko ya jiji la Nairobi, Machi 21, 2020. Gordwin ODHIAMBO / AFP
Matangazo ya kibiashara

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema kuwa watatu walioambukizwa ni raia wa Marekani, Cameroon na Burkina Faso, huku mmoja akiwa raia wa Kenya.

Maambukizi matatu yameripotiwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi na moja jijini Mombasa. watu 1,426 waliotangamana na ambao wanashukiwa kuambukizwa virusi hivyo wanatafutwa.

Hata hivyo wataalamu wa afya wanasema licha ya mikakati muhimu iliyotangazwa na Serikali kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, vita ya kuukabili itakuwa ngumu ikiwa wananchi hawataendelea kuelimishwa kuzingatia usafi na njia za kujikinga.

Kenya kwa sasa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwatafuta watu waliotangamana na watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Covid-19.

Hivi karibuni msemaji wa serikali, Cyrus Oguna, alitoa wito kwa watu ambao huenda wa walitangamana na wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo kufika katika kituo cha afya kilicho karibu nao.