Mgonjwa wa kwanza wa Covid-19 afariki dunia Tanzania
Serikali ya Tanzania imetangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Corona nchini humo. Mgonjwa huyo alikuwa mwanaume, raia wa Tanzania mwenye miaka 49 ambaye pia alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine.
Imechapishwa:
Mgonjwa huyo amefariki dunia katika kituo cha matibabu ya wagonjwa wa Corona huko Mloganzila katika mji mkuu wa kiuchumi wa Dar es Salaaam.
Jumatatu wiki hii Wizara ya Afya nchini Tanzania, ilitangaza wagonjwa wapya watato wa virusi vya Corona, hali inayofikisha idadi ya wagonjwa nchini humo kufikia 19 siku moja kabla ya kifo cha mgonjwa wa kwanza kutokea.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, wagonjwa hao wapya watano wote ni raia wa Tanzania.
Wagonjwa wawili ni kutoka visiwani Zanzibar na watatu kutoka Dar es Salaam.
UPDATE #COVID19Tanzania: 5 new POSITIVE cases; total 19 confirmed cases as of today. Out of these 1 person has recovered #JikingeWakingeWengine @TZMsemajiMkuu https://t.co/heQFNct6aT
Ummy Mwalimu, MP (@umwalimu) March 30, 2020
Nchini Tanzania, wagonjwa wa virusi hivyo wamebainika kutoka Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Kagera.
Wakati idadi ikipanda nchini Tanzania Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe leo Jumatatu ametangaza idadi ya wagonjwa nchini humo kufikia 50.
Nchini Uganda, rais Museveni ametangaza amri ya kutotoka nje usiku kwa siku 14 katika kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona, wiki mbili baada ya kupiga marufuku usafiri wa Umma.
Nchini Uganda mpaka sasa idadi ya maambukizi imefika watu 33.