DUNIA-CORONA-AFYA

Maambukizi ya virusi vya Corona kote duniani yapindukia Milioni tano

Sanduku za watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 wakisubiri kuzikwa katika makaburi ya Manaus, Brazil.
Sanduku za watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 wakisubiri kuzikwa katika makaburi ya Manaus, Brazil. MICHAEL DANTAS / AFP

Maambukizi ya virusi vya Corona kote duniani, vimeongezeka na kufikia zaidi ya Milioni tano, wakati huu China ikisema inaelekea kupata ushidni dhidi ya maambukizi haya.

Matangazo ya kibiashara

Hesabu iliyofanywa na Shirika la Habari la Ufaransa AFP  na chuo Kikuu cha Johns Hopkins University inaonesha kuwa, idadi imeongezeka licha ya mataifa mengi barani Ulaya virusi hivi vikionekana kupungua lakini vikiongezeka katika mataifa ya Latin America hasa nchini Brazil lakini pia Peru, Mexico na Chile.

Mbali na maambukizi hayo, watu wengine 328,000 kote duniani wamepoteza maisha kutokana na virusi hivi ambavyo vimeendelea kuleta hali ya sintofahamu duniani.

Nchini Marekani, idadi ya vifo imefika zaidi ya Elfu 93, huku kukiwa na wasiwasi kuwa hivi karibuni, huenda idadi hiyo itaongezeka na kufikia zaidi ya 100,000.

Baadhi ya mataifa barani Ulaya, kama Uhispania, Italia na Ufaransa shughuli zimeanza kurudi taratibu, huku India ikisema itafungua angaa lake ili safari za ndani ya nchi hiyo zianze ifikapo tarehe 25 mwezi huu.