DUNIA-WHO-CORONA-AFYA

WHO yasitisha majaribio ya dawa ya hydroxychloroquine kama tiba ya virusi vya Corona

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus. Christopher Black / World Health Organization / AFP

Shirika la Afya Duniani, WHO, limeonya kuwa huenda virusi vya Corona vikashuhudiwa tena kwa mara ya pili katika nchi ambazo virusi hivyo vimeanza kupungua, iwapo tahadhari za kiafya hazitaendelea kuzingatiwa.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa matukio ya dharura katika Shirika hilo Daktari Mike Ryan amesema kuwa, licha ya virusi hivyo kuonekana kuanza kupungua lakini vinaongezeka katika Amerika Kusini, Kusini mwa bara Asia na barani Afrika.

Wakati huo huo, WHO imesitisha kwa muda majaribio ya dawa inayotumiwa kutibu Malaria hydroxychloroquine kama tiba  ya virusi hivyo.

“Majaribio yanayofanyiwa dawa ya ugonjwa wa malaria Hydroxychloroquine ili kuona iwapo inaweza kutibu virusi vya Corona yamesitishwa kutokana na hofu ya usalama wake, “ Shirika la Afya Duniani WHO limesema katika taarifa.

Wiki iliopita, utafiti uliofanywa na jarida la tiba duniani Lancet ulibaini kwamba hakuna faida yoyote kwa kutumia dawa ya Hydroxychloroquine na kwamba utumizi wake unaweza kuongeza idadi ya vifo miongoni mwa wagonjwa hospitalini walio na maambukizi ya Corona.

Hydrochloroquine ni dawa salama ya kutibu ugonjwa wa malaria, baridi yabisi na Lupus, lakini hakuna majaribio yoyote ambayo yamependekeza matumizi yake kutibu Covid-19.

Hivi karibuni rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa anatumia dawa hiyo kuzuia virusi vya Corona.

Hata hivyo watafiti wanasemaa kwamba wagonjwa wa Covid-19 hawafai kutumia hydroxychloroquine.

Kufikia sasa Marekani imerekodi visa Milioni 1.7 vya maambukizi ya virusi vya Corona, na wagonjwa 353,00 wamepona ugonjwa huo ambao umeuwa watu 99,462.