WHO-CORONA-AFYA

WHO yatiwa wasiwasi na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona duniani

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kama Shirika hawana uwezo wa kuzilazimisha nchi kufuata ushauri wao.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kama Shirika hawana uwezo wa kuzilazimisha nchi kufuata ushauri wao. REUTERS/Denis Balibouse

Shirika la Afya duniani, linasema maambukizi ya virusi vya Corona yameongezeka kwa kipindi cha wiki moja iliyopita barani Ulaya, hali ambayo inazua wasiwasi wa kuendelea kushuhudiwa kwa maambukizi mapya.

Matangazo ya kibiashara

WHO inasema hatua za makusudi zinastahili kuchukuliwa kudhibiti hali hii ili kuepusha mataifa ya bara hilo kulemewa na ongezeko la virusi hivyo, wakati huu mataifa mengi yanapoanza kurejea katika hali ya kawaida.

Bara la Ulaya pekee limeripoti visa Milioni 2.6 vya maambukizi ya Corona, huku watu zaidi ya 195, 000 wakipoteza maisha.

Mapema wiki hii Shirika la Afya duniani, WHO lilionya kuendela kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona wakati huu nchi mbalimbali zinapoendelea kurejea katika hali ya kawaida.

Ufaransa maisha yameanza kurejea kawaida na kwa mara ya kwanza kulishuhudiwa tamasha la muziki na Mamilioni ya wanafunzi wamerejea Shuleni.

Nchini Uhispania mipaka imefunguliwa na hali ya hatari kuondolewa. Hata hivyo, wakati mataifa kadhaa ya Ulaya maisha yakianza kurejea taratibu, mataifa ya Amerika Kusini yameendelea kushuhudia ongezeko la maambukizi yakiongozwa na Brazil.