DUNIA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Idadi ya visa vipya yaongezeka duniani

Corona imeathiri mambo mengi katika nchi nyingi duniani.
Corona imeathiri mambo mengi katika nchi nyingi duniani. AFP/Pool/Bernd von Jutrczenka

Idadi ya kila siku ya maambukizi ya virusi vya Corona duniani imefikia rekodi mpya kwa visa 307,930, Shirika la Afya duniani, WHO, limethibitisha na kusema kuwa hali hiyo inatisha.

Matangazo ya kibiashara

Ongezeko kubwa zaidi limeonekana nchini India, Marekani na Brazil. India imerekodi visa vipya 94,372, Marekani visa vipya 45,523 na Brazil visa vipya 43,718, WHO imebaini kwenye wavuti yake.

Janga hilo pia limesababisha vifo vipya 5,537 katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufanya idadi ya vifo duniani kufikia 917,417.

Rekodi ya awali ya idadi ya kesi mpya katika muda wa saa 24 iliripotiwa Septemba 6 kwa visa 306,857. Rekodi ya vifo, ambayo ni 12,430, iliripotiwa Aprili 17.

Mlipuko wa virusi vya corona unaosababisha ugonjwa wa Covid-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.

Kufikia sasa kinachojulikana ni kuwa Covid-19, ni ugonjwa ambao unaothiri mfumo wa kupumua wa binadamu.

Dalili zake ni pamoja na homa kali, kukohoa ambako baada ya wiki moja muathiriwa anakabiliwa na tatizo la kupumua.