DUNIA-UN-CORONA-AFYA

Antonio Guterres: Viongozi wa dunia wameshindwa kuonyesha utashi kukabiliana na janga la Corona

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress. ©REUTERS/Carlo Allegri

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress amewaambia viongozi wa dunia kuwa wameshindwa kuonesha uongozi katika vita dhidi ya janga la Corona ambalo limewaambukiza watu zaidia ya Milioni 32 na kusababisha vifo ambavyo sasa vinakaribia Milioni Moja.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Guteress imekuja baada ya Marekani na China kulaumaiana wazi kwenye Mkutano wa Baraza la Usalama la Umpja wa Mataifa kuhusu janga hili.

Wakati huo huo India imerekodi visa vipya 86,052 vya maambukizi ya virusi vya Corona uchafuzi katika muda wa saa ishirini na nnezilizopita, kulingana na takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya india leo Ijumaa.

Kufikia sasa india ina visa milioni 5.82 vya maambukizi ya virusi vya Corona na vifo 92,290, baada ya vifo 1,141 kuthibitishwa katika muda wa saa ishirini na nne zilizopita.

Angalau vifo 1,000 vilirekodiwa kila siku nchini India katika wiki tatu zilizopita.

India ni nchi ya pili ulimwenguni iliyoathirika zaidi na mgogoro huu wa kiafya kwa idadi ya visa vya maambukizi, baada ya Marekani.

Brazil imerekodi visa vipya 32,817 vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi ya Corona na vifo vipya 831 vinavyotokana na janga hilo katika muda wa saa ishirini na nne zilizopita, wizara ya afya imesema hivi punde.

Kufikia sasa idadi ya maambukizi nchini Brazil ni zaidi ya milioni 4.6, na karibu jumla ya vifo 140,000 vimeripotiwa, kulingana na takwimu za serikali.

Brazil ni nchi ya pili kuathirika zaidi na mgogoro wa kiafya baada ya Marekani, kwa suala la maambukizi au vifo.

Hivi karibuni shirika la Afya Duniani, WHO, lilitoa wito kwa serikali mbalimbali za dunia na viongozi wa sekta mbalimbali za kiafya kuangazia kwa umakini afya na usalama wa wahudumu wa afya na wagonjwa, hasa kipindi hiki cha janga la Corona.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, WHO liliwataka wadau husika kuchukua hatua madhubuti kuwalinda wahudumu wa afya dhidi ya dhulma na maswala mengine yanayohatarisha usalama wao.