MAREKANI

Mike Huckabee,asema hatogombea urais wa Marekani katika uchaguzi wa mwaka 2012

(Photo : Reuters)

Gavana wa zamani wa jimbo la Arkansas nchini Marekani, Mike Huckabee ametangaza rasmi nia yake ya kutowania nafasi ya urais wa taifa hilo katika uchaguzi wa mwaka 2012.

Matangazo ya kibiashara

Huckabee, ambaye ni mfuasi wa chama cha Republican amekuwa akipewa nafasi kubwa na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini humo kuwa huenda chama chake kikamteua kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2012.

Akizungumza katika kipindi chake cha televisheni ya Fox News, Huckabee amesema kuwa nafsi yake bado haijaaamua kuwania uraisi hapo mwakani kwakuwa amekuwa akisita mara kwa mara kutangaza wazi endapo atawania nafasi hiyo au la kupitia chama cha Republican.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 2008, Huckabee aliwania nafasi hiyo kupitia chama chake lakini alishindwa na mpinzani wake John McCain aliyewania urais kupitia chama hicho na mgombea wa Democratic Barack Obama.

Tayari vuguvugu la viongozi kadhaa toka chama cha Republican limeanza kufukuta ndani ya chama hicho ambapo vikongozi kadhaa wamekuwa wakihusishwa na kutaka kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho akiwemo aliyekuwa mgombea mweza wa McCain Sarah Palin.

Mwezi wa nne mwaka huu rais Barack Obama alitangaza kuwa atawania tena nafasi hiyo kupitia chama chake cha Democratic ambacho kimeonesha kuwa na imani nae hasa baada ya kufanikiwa kumuua kiongozi wa mtandao wa kigaidi duniani Osama Bin Laden.