MAREKANI

Rais Obama asogeza mbele hotuba yake kwenye Bunge la Congress

REUTERS

Rais wa Marekani Barack Obama amelazimika kubadili tena tarehe ya kuwasilisha hotuba yake iliyolenga kueleza hali ya uchumi wa taifa hilo katika Bunge la Congress baada ya tarehe ya awali kupingwa na Spika wa Bunge John Boehner.

Matangazo ya kibiashara

Hatua ya kubadilishwa kwa tarehe kulikuja baada ya Spika wa Bunge Boehner kuweka bayana kuwa terehe 7 ya mwezi Septemba ambayo ilikuwa inatakiwa kutumiwa na Rais Obama itakuwa ni maalum kwa Chama Cha Repulican kufanya mdahalo wa wagombea wao wa urais.

Kutokana na ratiba hizo kuingiliana ndipo Spika Boehner akamtaka Rais Obama kutumia siku ya tarehe 8 ya mwezi Septemba kuwasilisha hotuba yake ambayo itakuwa inataja hatua ambazo zimepigwa na serikali katika kukuza uchumi wa taifa hilo.

Rais Obama anatarajiwa kuweka bayana mikakati yao katika kuimarisha uchumi wa taifa hilo pamoja na kushughulikia suala la ajira ambapo serikali yake imekowa ikikosolewa vikali na wananchi walio wengi wanaohaha kusaka ajira.

Rais Obama ambaye amekuwa akihaha kuhakikisha anakabiliana na tatizo la ajira kwenye nchi yake alitaka kutumia fursa hiyo kuwaambia Wabunge wa Congress namna ambavyo suluhu ya kudumu itakavyopatikana juu ya suala hilo linaloumiza vichwa vya wengi.

Hotuba ya Rais Obama baada ya kugonga mwamba kutolewa tarehe 7 ya mwezi Septemba ambayo itakuwa siku ya jumatano sasa imepelekwa siku ya Alhamisi ambapo wabunge wa Congress watajua kinagaubaga namna ambavyo serikali imepiga hatua.

Rais Obama atatumia fursa hiyo kujibu hoja za wabunge wa Republican ambao wamekuwa vinara wa kukosoa sera za serikali yake wakiamini ameshindwa kutekeleza masuala mengi ambayo aliyaahidi kabla ya uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.

Wananchi wengi wanahamu ya kujua suala la ajira lilivyoshughulikiwa wakati huu ambapo takwimu zinaonesha ukosefu wa ajira umechupa na kufikia asilimi tisa na kuwafanya raia waanze kulalama na kuhoji sera ambazo zinatumiwa na serikali ya Rais Obama.