PALESTINA-MAREKANI

Palestina yaendelea kusisitiza mpango wake wa kutaka kupewa uanachama wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa

Mkutano wa baraza la Umoja wa mataifa ulioketi hivi karibuni kuijadili Palestina
Mkutano wa baraza la Umoja wa mataifa ulioketi hivi karibuni kuijadili Palestina UN Photo/Paulo Filgueiras

Serikali ya Mamlaka ya Palestina kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje Riyad Al maliki amesema kwa sasa wanaendelea na mpango wao wa kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kupata uanachama wa Umoja wa Mataifa UN bila kujali itawachukua muda gani.

Matangazo ya kibiashara

Al Maliki amewaambia wanahabari kuwa kwa sasa wamepata nguvu na kuhisi watafanikiwa kwenye mpango wao wa kuwa wanachama wa UN kutokana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughilikia Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kuwatambua.

Msimamo huo umegongelewa msumari na Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa UN Riyad Mansour ambaye anasema wataendelea na shinikizo la kutaka uwanachama.

Suala la Palestina kutaka kupewa uanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeendelea kuwa gumzo kwa mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza na Ufaransa ambao wao wameweka wazi msimamo wao kuhusu Palestina ya kwamba hawataunga mkono ombi hilo.

Kikao cha baraza la usalama kinatarajiwa kuketi juma lijalo kuamua hatma ya Palestina ambapo nchi zenye kura ya turufu watapiga kura kuamua kuipa au kutokuipa uanachama nchi ya Palestina.

Hatua ya hapo juzi ya UNESCO kuamua kuitambua Palestina kama mjumbe wake wa kudumu ilisababisha Marekani kusitisha msaada wa kifedha katika shirika hilo huku Israel nayo ikaamua kutangaza rasmi kuendelea na ujenzi wa makazi ya kudumu katika eneo la Jerusalem.