MAREKANI

Daktari wa hayati Michael Jackson athibitishwa kuwa na hatia ya mauaji ya kutokusudia

Daktari wa hayati Michael Jackson Conrad Murray
Daktari wa hayati Michael Jackson Conrad Murray REUTERS / Irfan Khan

Daktari binafsi wa hayati Michael Jakson, Daktari Conrad Murray amekutwa na hatia ya kosa la mauaji bila kukusudia na mahakama moja mjini Los Angeles Marekani, kutokana na kifo cha mfalme wa pop Juni 25 mwaka 2009.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya siku mbili wakijadili kesi hiyo hatimae baraza la wazee kumi na wawili wa mahakama wamefikia uamuzi huo uliosomwa mbele ya familia ya hayati Michael Jackson.

Wakati hukumu hiyo ikisomwa ndugu wa Michael Jackson walishindwa kuvumilia na kuanza kumiminikwa na machozi na dada yake Jackson, Latoya Jackson alipaza sauti ya furaha wakati Daktari Murray akionekana mwenye uchungu.

 

Jaji Michael Pastor aliamuru kuwekwa kizuizini na kuonyesha kwamba mwenendo wa daktari huyo unahatarisha usalama wa umma.

Mashabiki wa hayati Michael Jackson waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo nnje ya mahakama walionyesha furaha yao na kusema kwamba hatimae sheria imefuata mkondo wake.

Murray, 58, anaweza kukabiliwa na adhabu ya kwenda gerezani kwa miaka minne na kupoteza leseni yake uweledi, atakaposomewa hukumu yake tarehe 29 mwezi Novemba.