PAKISTAN-MAREKANI-NATO

Serikali ya Pakistan yaikataa ripoti ya uchunguzi uliofanywa na majeshi ya Marekani na NATO

Wanajeshi wa Pakistan wakiwazika wanajeshi wenzao waliouawa kwenye shambulio la Nov 26
Wanajeshi wa Pakistan wakiwazika wanajeshi wenzao waliouawa kwenye shambulio la Nov 26 REUTERS

Serikali ya Pakistan kupitia jeshi la nchi hiyo imekataa kupokea ripoti ya pamoja ya Marekani na Majeshi ya nchi za kujihami NATO kuhusiana na tukio la mwezi wa kumi na moja kwenye mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan ambapo wanajeshi 24 wapakistan waliuawa. 

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliyotolewa na jeshi la nchi hiyo imesema kuwa ripoti ambayo imetolewa na Marekani na NATO imeshindwa kueleza ukweli wa namna ambavyo tukio hilo limetokea na kwamba ni fupi mno kulingana na tukio lenyewe.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kamwezi haitaikubali ripoti hiyo kwakuwa haijawatendea haki familia ambazo zimepoteza ndugu zao katika shambulio hilo la anga huku ikishindwa kueleza hatua ambazo zitachukuliwa dhidi ya wanajeshi waliohusika kwenye shambulio hilo.

Serikali ya Marekani kupitia kwa Brigedia Jenerali Stephen Clark ambaye alihusika katika uchunguzi huo alikiri wanajeshi wao kutumia ramani ambayo hakikuwa sahihi na hivyo kushindwa kuelewa kwa ufasaha mpaka wa Pakistan na Afghanistan uliopelekea shambulio hilo.

Jenerali Clark ameongeza kuwa shambulio hilo la kimakosa lilitokana na majeshi ya Pakistan kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu mipaka yake na maeneo ambayo huwa wanayalinda kiasi ambacho usiku wa tarehe 26 mwezi wa kumi na moja kuhisi kwamba wanavamiwa na hivyo kuamua kuita msaada wa mashambulizi ya anga yaliyoua wanajeshi wake 23.

Kwa upande wake majeshi ya NATO yamekiri nayo kuhusika katika shambulio hilo wakisema kuwa ushirikiano wao na yale ya Marekani haukuwa mzuri hatua iliyopelekea kufanyika kimakosa kwa shambulio hilo.