MAREKANI

Newt Gingrich ajitoa kwenye mbio za kusaka mgombea wa urais katika Chama Cha Republican

Spika wa zamani wa Bunge nchini Marekani Newt Gingrich wakati anaanza harakati za kutaka kuwa Mgombea wa Urais wa Chama Cha Republican
Spika wa zamani wa Bunge nchini Marekani Newt Gingrich wakati anaanza harakati za kutaka kuwa Mgombea wa Urais wa Chama Cha Republican REUTERS/Dan Anderson

Spika wa zamani wa Bunge nchini Marekani Newt Gingrich ametangaza kujiondoa kwenye mbio za kusaka tiketi ya kuwa Mgombea wa Urais katika Chama Cha Republican kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba mwaka 2012.

Matangazo ya kibiashara

Gingrich ametangaza uamuzi huo na kusema amejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho cha ndani ya Chama Cha Republican lakini ameahidi kuendelea kuwa mwananchi mwema ambaye yupo tayari kushiriki kwenye maendeleo ya nchi hiyo.

Spika huyo wa zamani wa Bunge amesema hana nia wala lengo la kuondoka katika Chama chake cha Republican na atamuunga mkono mgombea ambaye atapishwa na wanachama wa chama hicho kubeba bendera ya chama hicho.

Gingrich ameweka bayana kucha mbio za kuwa mgombea wa uchaguzi hakuna maana yeye atakuwa si mwananchi wa Marekani mwenye uanachama halali wa Chama cha Republican anachoamini sera zake.

Gingrich anafuata nyayo za Mgombea mwingine wa Chama Cha Republican Rick Santorum ambaye yeye alitangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais mapema zaidi baada ya kuona nafasi ya yeye kushinda ni ndogo.

Spika huyo wa Bunge wa zamani mwenye umri wa miaka 68 amefikia uamuzi huo mgumu baada ya kuona upepo ushindi kwa upande wake hauvumi kwani ameshinda kwenye majimbo mawili tu kwenye kura za maoni.

Uamuzi huo wa Gingrich unatoa nafasi kwa wagombea wawili wa Chama Cha Republican Ron Paul na Mitt Romney kuendelea kuchuana kujua nani ataenda kupambana na Rais Barack Obama mwezi Novemba mwaka huu.

Romney ndiye ambaye anapigiwa chapuo ya kuwa mgombea kupitia Chama Cha Republican kutokana na kushinda kwenye majimbo mengine katika kura za maoni ukilinganisha na mpizani wake Paul.