Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ashutumu Mataifa yanayoendelea kuwasaidia waasi wa Congo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amesema kuwa mataifa ya kigeni bado yameendelea kusaidia Makundi ya Waasi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuwa yatalipa kutokana na Machafuko wanayoendelea kuyachochea nchini humo.
Imechapishwa:
Ban ametoa Onyo hilo, hata hivyo bila kuyataja kwa majina Mataifa yanayodaiwa kuunga mkono Waasi wa M23.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukidai kuwa Rwanda na Uganda zimekuwa zikiwapa silaha Waasi wa M23 wakiwa katika Operesheni zao dhidi ya Vikosi vya Serikali Mashariki mwa Congo, huku Mataifa hayo yakikana kuhusika na shutma hizo.
Ban amesema kuwa Mjumbe maalum atakayewakilisha nchi za ukanda wa Maziwa makuu ambaye amepanga kumchagua atafanya kazi ya kuhakikisha kuwa hakuna nchi inayoingialia maswala ya ndani ya nchi nyingine na kuhakikisha kuwa vitisho vya makundi ya watu wenye silaha yanakoma katika ukanda huo.
Ban amefafanua zaidi juu ya mpango wake wa kupeleka kikosi maalum cha kijeshi kitakachofanya kazi na MONUSCO ili kuongeza nguvu ya Operesheni.