VENEZUELA

Mazishi ya Rais wa Venezuela Hugo Chavez kufanyika ijumaa hii

Raia wa Venezuela wamejitokeza kwa wingi kuuona mwili wa Kiongozi wao Hugo Chavez ambao uliokuwa umelazwa katika ikulu ya nchi hiyo. Mwili wa Kiongozi huyo unatarajiwa kuhifadhiwa kwa ajili ya kumbukumbu na Raia watapata nafasi ya kufika eneo la makumbusho atakalokuwa amehifadhiwa.

Reuters
Matangazo ya kibiashara

Zoezi la kutoa heshima za mwisho kwa Chavez limeongezwa muda kwa siku saba zaidi baada ya shughuli za maziko ya hii leo ijumaa.

Viongozi mbalimbali wa kimataifa wameendelea kuwasili nchini humo kuhudhuria mazishi ya kiongozi huyo ambaye alikuwa akikabiliwa na maradhi ya saratani kwa takribani miaka miwili na alikuwa akipata matibabu nchini Cuba kwa kipindi cha miezi miwili na alifanyiwa upasuaji mara ya nne.

Spika wa Bunge la Venezuela Diosdado Cabello amesema Makamu wa Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro ataapishwa kuwa Rais wa mpito baada ya shughuli za mazishi kukamilika na ataitisha uchaguzi wa rais ndani ya siku 30.

Maduro ambaye atashika nafasi ya Urais kwa muda anatarajiwa kupambana na Henrique Capriles ambaye aliangushwa na Hugo Chavez katika uchaguzi wa mwezi oktoba mwaka jana.