AFGHANISTANI-MAREKANI

Shambulio la kujitoa mhanga lasababisha vifo vya watu 9 nchini Afghanistan

(Carte: RFI)

Mlipuko wa bomu la kujitoa muhanga katika Wizara ya Ulinzi mjini Kabul nchini Afghanistan umesababisha vifo vya watu takribani tisa na kujeruhi wengine zaidi ya ishirini jumamosi hii. Tukio hilo limeripotiwa kutokea wakati Waziri mpya wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel alipotembelea mji huo.

Matangazo ya kibiashara

Kundi la kigaidi la Taliban limekiri kuhusika na shambulio hilo na kusema hawakutaka kumshambulia moja kwa moja Hagel bali walitaka kuonyesha kuwa wanaweza kuishambulia Kabul hata kama kiongozi wa Marekani akiwa katika eneo hilo.

Aidha katika mji wa Khost kumeripotiwa kutokea mlipuko mwingine hii leo na taarifa zinasema watoto nane na polisi mmoja wamepoteza maisha katika tukio hilo.

Vikosi vya kijeshi vya Afghanistan vinatarajiwa kuchukua jukumu la ulinzi katika maeneo yote ya nchi wakati vikosi vya nje vitakapoanza kuondoka lakini maswali yamekuwa yakiibuka iwapo wataweza kukabiliana ipasavyo na wapiganaji wa Kitaliban.