PARAGUAY

Horacio Cartes aibuka kinara katika uchaguzi wa Urais nchini Paraguay

AFP PHOTO/Pablo PORCIUNCULA

Mfanyabiashara anayemiliki utajiri mkubwa nchini Paraguay Horacio Cartes ameibuka mshindi kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais wa nchi hiyo huku akionekana kuwavutia wapiga kura wengi kutokana na kuahidi kushughulikia biashara haramu ya mihadarati.

Matangazo ya kibiashara

Horacio Cartes amefanikiwa kupata asilimia 45.91 ya kura zote ambazo zimepigwa huku mpinzani wake mkubwa Efrain Alegre akiambulia asilimia 36.84.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Paraguay Alberto Ramirez ndiye ametangaza matokeo hayo ambapo yamepokelewa kwa furaha kubwa na wafuasi wa Cartes ambao wamejitokeza kwenye mitaa mbalimbali kushangilia ushindi huo.

Alegre kutoka Chama Cha Kiliberali amekubali kushindwa kwenye kinyang'anyiro hicho na kumpongeza mshindani wake Cartes na kumtakia kila la kheri katika kuhakikisha anatimiza ahadi alizozitoa kwa wananchi.

Asilimia 40 ya wananchi wa Paraguay wanaishi kwenye umasikini mkubwa huku biashara haramu ya dawa za kulevya ikiwa imeshamiri katika nchi hiyo hali inayochangia kukithiri kwa vitendo vya uhalifu.