MAREKANI-KOREA KASKAZINI

Marekani kumtuma mjumbe wake Korea Kaskazini kumwokoa raia wake

Marekani inasema itamtuma mjumbe wake nchini Korea Kaskazini kuomba kuachiliwa huru kwa raia wake anayezuiliwa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Robert King, mjumbe wa Marekani anatarajiwa kuwasili Pyongyang siku ya Ijumaa kujaribu kushawishi kuachiliwa huru kwa Kenneth Bae mwenye umri wa miaka 45 kwa sababu za kibinadamu.

Bae aliye na asili ya Korea alihukumiwa jela miaka 15 mwezi Mei mwaka huu baada ya kupatikana na kosa la kuipindua serikali ya Korea Kaskazini kwa kutumia makundi ya wafanyibiashara.

Familia ya Bae inasema kuwa afya yake ni mbaya baada ya kusumbuliwa na kifua Kikuu na kupata tatizo la moyo na kwa sasa anapata matibabu hospitalini.

Bae ambaye kwa jina lingine anaitwa Pae Jun-ho alikamatwa mwezi Novemba mwaka 2012 wakati akijaribu kuingia katika bandari ya Rason karibu na mpaka wa China.

Miongoni mwa raia wengine ambao wamewahi kukamatwa na kufungwa nchini humo na baadaye kuachiliwa huru ni pamoja na Eddie Jun Yong-su, Aijalon Mahli Gomes, Robert Park na Laura Ling/Euna Lee.

Mbali na Robert King, wajumbe wengine wa amani ambao wamekuwa wakijihusisha na juhudi za kuwaokoa wananchi wake wanaokamatwa ni pamoja na rais wa zamani Jimmy Carter na Bill Clinton.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Washingtn DC na Pyongyang kutokana na raia wa Marekani wakiwemo Wahubiri wa dini ya Kikristo na waandishi wa habari kukamatwa kila wakati umeendelea kuyumba.