URUSI-UKRINE-Siasa

Urusi inajianda kuondoa jeshi lake kwenye mpaka na Ukraine

Rais wa Urusi, Vladimir Poutine (Katikati) akiahidi kuondoa wanajeshi wake kwenye mpaka wa nchi yake na Ukraine.
Rais wa Urusi, Vladimir Poutine (Katikati) akiahidi kuondoa wanajeshi wake kwenye mpaka wa nchi yake na Ukraine. REUTERS/Mikhail Klimetyev/RIA Novosti/Kremlin

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa tayari ameyaamuru majeshi ya nchi yake kuondoka katika mpaka wake karibu na nchi ya Ukraine na kurejea katika kambi zake za kijeshi.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo inakuja wakati huu Ukraine ikitarajiwa kufanya uchaguzi wake hivi karibuni ikilenga kumaliza mgogoro unaoendelea nchini humo ambao urusi imekuwa ikilaumiwa kuuchochea na mataifa ya magharibi.

Hata hivyo mataifa ya umoja wa kujihami wa nchi za magharibi NATO bado hayaamini kama urusi itaondoa majeshi yake. Katibu mkuu wa Umoja wa kujihami wa nchi za magharibi NATO, Fogh Rasmussen, amesema iwapo Urusi itayaondoa majeshi yake kwenye mpaka na Ukraine itachangia kwa kuleta utulivu nchini Ukraine.

“Mpaka sasa hatujashuhudia majeshi yoyote yakiondoka, lakini ninakiriri wazi kwamba kuondoka kwa majeshi ya urusi itakuwa ni hatua muhimu na mchango thabiti katika harakati za kumaliza mgogoro nchini Ukraine, amesema Rasmussen.

Wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine.
Wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine. REUTERS/Thomas Peter

Katika hatua nyingine Marekani inasema kuwa Urusi huenda inaendeleza ahadi zake za uongo kwani imekuwa ikiahidi kufanya hivyo mara kadha lakini hadi sasa hakuna ahadi iliyotekelezwa.

Msemaji wa ikulu ya marekani, Jay Carney, amesema kauli ya Urusi imejaa tu uongo.
“Mpaka wakati huu hatujaona hata dalili za majeshi kuondoka katika maeneo karibu na Ukraine licha ya Urusi kuahidi kufanya hivyo mara kwa mara hapo awali kama mnavyofahamu”, amesema Carney.

Urusi imekua ikilaumiwa kuendelea kuchochea vurugu nchini Ukraine kwa kuwaunga mkono waasi wa mashariki mwa Ukraine wanotaka maeneo ya mashariki kujitenga na Ukraine na kujiunga naUrusi.