SYRIA

Obama aomba Congress Dola Milioni 500 kuwasaidia waasi Syria

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack Obama Reuters/路透社

Rais wa Marekani Barrack Obama ameliomba bunge la Congress kupitisha bajeti ya Dola Milioni 500 ili kuwafadhili na kuwapa mafunzo waasi wenye msimamo wa kadri wanaopambana na serikali ya Syria.

Matangazo ya kibiashara

Ikulu ya Marekani inasema, fedha hizo zitawawezesha waasi hao kununua silaha za kujilinda dhidi ya wanajeshi wa rais Bashar al Assad.

Aidha, Marekani inasema fedha hizo zitasaidia katika harakati za kupambana na wapiganaji wa Kislamu nchini Iraq wa ISIS ambao wanaedelea kupambana na serikali ya Iraq.

Nchini Syria, zaidi ya watu 100,000 wamepoteza maisha nchini humo kwa zaidi ya miaka mitatu katika mapambano dhidi ya serikali ya serikali ya Assad.

Uharibifu nchini Syria
Uharibifu nchini Syria REUTERS/Omar Sanadiki

Rais Obama amekuwa katika shinikizo kutoka kwa baadhi ya wabunge wa Congress kuongeza uungwaji mkono  kwa wapinzani na haijafahamika vema ikiwa watakubali au la kupitisha bajeti hiyo.

Mshirika wa karibu wa Syria ambaye ni Urusi, imeshtumu hatua hiyo ya Marekani kwa kile inachosema kuwa Marekani inaweza kutumia fedha hizo kwa kazi nyingine badala ya kuwapa waasi hao.

“Wamarekani wanafuata njia yao wenyewe, wamekuwa wakiendelea kuichoma Syria badala ya kufanya jitihada za kupata suluhu la kisiasa,” Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin amewaambia waandishi wa Habari.

Waasi wa Syria
Waasi wa Syria REUTERS/Houssam Abo Dabak

Ikiwa bunge la Congress litapitisha Bajeti hiyo, Marekani itawapa mafunzo waasi hao ili kujilinda dhidi ya wanajeshi wa serikali ya Bashar Al Assad.