MAREKANI-CUBA-DIPLOMASIA

Barack Obama atangaza uhusiano mpya na Cuba

Baada ya serikali ya Cuba kutangaza kumuachilia huru, Alan Gross, raia wa Marekani, rais wa Marekani, Barack Obama ametangaza Jumatano Desemba 17 kwamba alimuomba Waziri wa mambo ya nje, John Kerry, kuanzisha mazungumzo na Cuba.

Rais Barack Obama akizungumza kwa simu na Alan Gross, raia wa Marekani aliye achiliwa huru na Cuba, Desemba 17 mwaka 2014, siku ya kihistoria ya kuanzishwa kwa uhusiano mpya kati ya Marekani na Cuba.
Rais Barack Obama akizungumza kwa simu na Alan Gross, raia wa Marekani aliye achiliwa huru na Cuba, Desemba 17 mwaka 2014, siku ya kihistoria ya kuanzishwa kwa uhusiano mpya kati ya Marekani na Cuba. REUTERS/Pete Souza/White House
Matangazo ya kibiashara

Barack Obama amebaini kwamba mazungumzo hayo ni hatua mojawepo ya kusitisha uhasama kati ya Marekani na Cuba uliyodumu zaidi ya miaka hamsini, na kufufua uhusiano wa kidiplomasia.

Katika hotuba yake kwenye televisheni, Barack Obama amesema amemuomba Waziri wa mambo ya nje, John Kery kuanzisha mazungumzo na Cuba kuhusu uhusiano wa kisiasa. Marekani imepanga kufungua ubalozi wake katika mji mkuu wa Cuba, La Havane, baada ya ubalozi huo kufungwa tangu Januari mwaka 1961.

Kwa upande wake rais wa Cuba, Raul Castro, amehotubia raia wake kupitia televisheni mbalimbali katika kisiwa hicho cha Cuba, akithibitisha kwamba kumeanzishwa upya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba. Castro amebaini kwamba suala ambalo limesalia ni vikwazo viliyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.

Hata hivyo Barack Obama ametangaza kwamba amepanga kukutana na wabunge wa Marekani ili kujadili namna ya kuondoa vikwazo hivyo. Jumatano Desemba 17 Jioni, Ikulu ya White House imebaini kwamba ingelifurahia vikwazo hivyo viondolewe kabla ya muhula wa pili wa Obama kutamatika mwaka 2017.

" Nadhani tunaweza kusaidia zaidi raia wa Cuba katika majadiliano na serikali ya La Havana, amesema Obama. " Siasa inayoendeshwa na Washington katika miongo ya hivi karibuni kuhusiana na Cuba imekuwa na athari kidogo," ameongeza Obama, na kutangaza pia kwamba Marekani itaiondoa Cuba kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi.

Barack Obama pia alimshukuru Papa Francis, ambaye alifanya kazi kubwa ya kukutanisha viongozi wa mataifa hayo mawili ili kufufua uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kwa upande wake, Papa ameonyesha " furaha yake" kwa "uamuzi huo wa kihistoria".