CUBA-MAREKANI-WAFUNGWA-SHERIA-HAKI

Cuba yawaachia huru wafungwa wa kisiasa

Marekani imetangaza jana Jumanne Januari 6 mwaka 2015 kwamba Cuba imewaachia huru wafungwa wa kisiasa. Orodha ya wafungwa wa kisiasa 53 imewekwa wazi na Marekani, ambayo haikupendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu wanasiasa hao wa upinzani.

Maandamano ya mshikamano pamoja na wapinzani kutoka Cuba katika miji ya Miami na Florida, Desemba 30 mwaka 2014.
Maandamano ya mshikamano pamoja na wapinzani kutoka Cuba katika miji ya Miami na Florida, Desemba 30 mwaka 2014. REUTERS/Francisco Alvarado
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, amekaribisha uamzi huo wa Cuba na kuitolea wito kuendelea katika njia hiyo hasa kuwaachia wafungwa wote wa kisiasa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI mjini Washington, Anne-Marie Capomaccio, idadi ya wafungwa wa kisiasa walioachiwa huru haijajulikana, hata Marekani ambayo imekaribisha uamzi wa La Havane haikupendelea kutoa majina ya watu hao.

Msemaji wa John Kerry, amesema Marekani na Cuba zimeamua kujizuia kutoa majina ya wafungwa hao wa kisiasa walioachiwa huru, huku akisema kwamba baadhi yao bado wanazuiliwa jela.

Kama rais wa Cuba, Raul Castro amechukua uamzi wa kuwaachia huru wafungwa kadhaa wa kisiasa, ni katika makubaliano ya kuheshimu ahadi iliyotolewa na serikali ya Cuba kwa Marekani na Vatican wakati wa mazungumzo yaliofuatia tangazo la tarehe 17 Desemba mwaka 2014. Hata hivyo kuachiliwa huru kwa wafungwa hao wa kisiasa hakuhusiani na sharti la kuweka sawa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Washington na La Havane.

Haijajulikana iwapo uamzi huo wa Cuba ulichukuliwa kufuatia ombi la Seneta kutoka chama cha Republican nchini Marekani, mwenye asili ya Cuba, Marco Rubio, ambaye alimuomba hivi karibuni rais wa Marekani Barack Obama kutothubutu kufufua uhusiano na Cuba kama wanasiasa wote wa vyama vya upinzani wanaozuiliwa jela watakua hawajaachiliwa huru.