MAREKANI-SYRIA-SIASA

John Kerry: " Marekani hatimae itajadili na Assad"

Picha ya Rais Bashar al-Assad iliobandikwa katika kumbukumbu yamaadhimisho ya miaka minne ya vita nchini Syria, katika mji wa Damascus, Machi 15 mwaka 2015.
Picha ya Rais Bashar al-Assad iliobandikwa katika kumbukumbu yamaadhimisho ya miaka minne ya vita nchini Syria, katika mji wa Damascus, Machi 15 mwaka 2015. REUTERS/Omar Sanadiki

Katika mahojiano na televisheni na CBS News, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, ametangaza kwamba Marekani " hatimaye" itajadili na Bashar Al Assad kuhusu serikali ya mpito nchini Syria.

Matangazo ya kibiashara

Marekani imefuta kauli yake kuhusu utawala wa Assad. Marekani imekua ikisema kwamba Assad amepoteza uhalali wa mamlaka yake na anatakiwa kuondoka Madarakani. Katika mahojiano yaliyorushwa hewani kwenye televisheni CBS Jumapili Machi 15, miaka minne baada ya kuanza kwa mgogoro wa Syria, John Kerry ameonesha msimamo wa utawala wa Marekani. " Tutajadili tu", amesema waziri wa mambo ya nje wa Marekani. " Tulitaka kujadili katika mfumo wa mchakato wa Geneva", ameongeza John Kerry.

Marekani imeonekana kupunguza msimamo wake dhidi ya Bashar Al Assad kufuatia kuongezeka kwa mapigano yanayoendeshwa na kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu.

John Kerry ameeleza kuwa nchi nyingine zilikuwa zikitafakari njia ya kuzindua mchakato wa kidiplomasia ili kukomesha vita. " Ili kushawishi utawala wa Assad kujadili, tunapaswa kumueleza wazi kwamba sote tuna nia ya kutafuta ufumbuzi wa kisiasa na kubadili hesabu zake juu ya mazungumzo", ameelezea Kerry. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani hajaondoa uwezekano " wakutumia nguvu ili kumshinikiza Assad kushiriki mazungumzo na upinzani".

Mazungumzo ya hivi karibuni yaliofanyika mjini Geneva mwaka jana kati ya serikali ya Syria na wawakilishi wa upinzani yalifeli. Tangu wakati huo, hakuna mkutano mpya uliopangwa kufanyika.