MAREKANI-IRANI-ISRAELI-NYUKLIAp-USALAMA

Mazungumzo yanaendelea kati ya Marekani na Iran

Iran na mataifa yenye nguvu hatimae wamekumbaliana hadi kufikia tarehe 1 Julai mwaka 2015 wawe wameshafikia makubaliano ya jumla juu ya nyuklia ya Iran.
Iran na mataifa yenye nguvu hatimae wamekumbaliana hadi kufikia tarehe 1 Julai mwaka 2015 wawe wameshafikia makubaliano ya jumla juu ya nyuklia ya Iran. REUTERS/Joe Klamar

Marekani na Iran kwa siku ya pili leo wameendelea na mazungumzo ya kufikia mwafaka kuhusu mradi wa Nyuklia wa Iran.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif ambao wanakutana mjini Lausanne nchini Uswizi wameapa kufanya kila kinachowezakana kuhakikisha kuwa wanapata mwafaka kufikia mwisho wa mwezi huu.

Leo Jumanne, wawili hao wamekuwa wakipitia na kujadili njia ya kufikia mkataba wa namna ya kukabiliana na mradi huu wa Nyuklia ambao Mataifa ya Magharibi yanasema, Iran inautumia kutengeza silaha za maangamizi.

Ikiwa mkataba utafikiwa mwisho wa mwezi huu, utatiwa saini mwisho wa mwezi wa Juni na kuanza kutekelezwa kuanzia tarehe moja mwezi Julai mwaka huu.
Hata hivyo, mwanadiplomasia mmoja wa Marekani ambaye anahudhuria mazungumzo hayo amenukuliwa akisema kuwa Iran bado ina maamuzi mbele yake ili kufikia mkataba huo.

Wajumbe wengine kutoka Mataifa ya Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambao pia wanashiriki katika mazungumzo hayo wanatarajiwa kuwasili mjini Lausanne baadaye juma hili kuendelea na mazungumzo hayo.

Iran imeendelea kusisitiza kuwa mradi wake si wa kutengeneza silaha za maangamizi kwa lengo la kuivamia Israel, badala yake ni wa amani ili kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.