MAREKANI-CUBA

Obama na Castro wakutana na kuweka Historia

Rais wa Marekeni Barrack Obama na mwenzake wa Cuba Raul Castro wamekutana na kusalimiana wakati wa mkutano wa viongozi wa nchi za Americas nchini Panama.

Raul Castro na Barack Obama
Raul Castro na Barack Obama REUTERS/Panama Presidency
Matangazo ya kibiashara

Hii ni hatua kubwa inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili ambazo kwa zaidi ya miaka hamsini zimekuwa katiak vita baridi.

Viongozi hawa mawili waliwahi pia kusalimia na kukutana wakati wa mazishi ya rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini Nelson Mandela mwaka 2013.

Obama na Raul waliketi pamoja wakati wa mkutano huo wa marais wa eneo la Americas na siku ya Jumamosi watakutana pembezoni mwa mkutano huo kujadili maswala muhimu kati ya nchi zao.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Cuba kuhudhuria mkutano huo wa viongozi wa Americas ndani ya miaka 21 hatua iliyopongezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

Marekani na Cuba zilisitisha ushirikiano wa kidiplomasia mwaka 1961 na mkutano wa viongozi hawa unaangaziwa na wachambuzi wa mambo kuwa mwanzo mpya wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili umefika.

Mwezi Desemba mwaka jana, Cuba na Marekani zilitangaza kuwa zilikuwa tayari kumaliza tofauti zao na kuanza kushirikiana tena.

Wakati wa mkutano huo siku ya Jumamosi, miongoni mwa maswala muhimu yatakayojadiliwa ni ufunguzi wa ubalozi wa nchi hizo mbili pamoja na kuiondoa Cuba katika orodha ya Marekani ya mojawapo ya nchi inayofadhili ugaidi.

Maamuzi yoyote yatakayoafikiwa, itabidi yaidhinishwe na bunge la Congress kwa muda wa siku 45 zijazo.