BRAZIL-MAANDAMANO-USALAMA

Brazil: maelfu ya waandamanaji dhidi Dilma Rousseff

Maelfu ya raia wa Brazil wameandamana Jumapili Agosti 16 wakidai uchaguzi mpya au kujiuzulu kwa rais kutoka mrengo wa kushoto Dilma Rousseff, ambaye anakabiliwa na makosa matatu ya kiuchumi, kisiasa na kashfa ya rushwa.

Katika mji wa Rio de Janeiro kama katika miji kadhaa ya Brazil, wapinzani wamefanya maandamano dhidi ya rais Dilma Rousseff na kashfa ya rushwa.
Katika mji wa Rio de Janeiro kama katika miji kadhaa ya Brazil, wapinzani wamefanya maandamano dhidi ya rais Dilma Rousseff na kashfa ya rushwa. REUTERS/Paulo Whitaker
Matangazo ya kibiashara

Takriban raia 900,000 wa Brazil wamefanya maandamano Jumapili Agosti 16 wakidai rais Dilma Rousseff, aondoke madarakani.

Kiongozi wa upinzani Aecio Neves ameshiriki katika maandamano hayo, ambayo yanaonekana kuzidisha nguvu katika nyanja ya kisiasa kwa uhamasishaji dhidi ya utawala.

Waandaaji ikiwa ni pamoja na mashirikia ya kiraia kutoka mrengo wa kulia yakiungwa mkono na baadhi ya vyama vya upinzani, wametolea wito wafuasi wao kujitokeza kwa wingi mitaani katika zaidi ya miji 200 ya nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.

Wandaaji walikua na matumaini ya kuhamasisha kama ilivyokua wakati wa maandamano kama hayo mwezi Machi (waandamanaji angalau milioni moja) na mwezi Aprili (waandamanaji 600,000) walijitokeza mitaani.

Lakini mapema Jumapili mchana, uhamasishaji umeonekana mdogo. Waandamanaji walikuwa kati ya 137,000 (kwa mujibu wa polisi) na 604.000 (kwa mujibu wa waandaaji), kulingana na idadi ya awali ambayo ingeweza kuongezeka wakati wa mchana, hasa pamoja na maandamano ya Sao Paulo, ngome kuu ya upinzani na mji wenye wakaazi wengi nchini Brazil, ambao una wakaazi milioni 11.

Wakiwa wamevaa jezi zenye rangi ya kijani na njano za timu ya taifa ya soka "Selecao", wandamanaji hao wameandamana tangu asubuhi katika eneo la katikati la mji mkuu wa Brasilia, Belo Horizonte (Kusini Mashariki), Recife (Kaskazini Mashariki), Salvador Bahia (Kaskazini Mashariki) na Belem (Kaskazini).

Waandamanaji hao walikua wamebeba mabango yenye maandishi "Ondoka Dilma!" na "hapana kwa rushwa!", kwa uchache watu 25,000 wameandamana katika mji wa Brasilia.

" Tutapinga mpaka mwisho. Hadi Rais ajiuzulu. Anapaswa kuondoka moja kwa moja na aiache nchi hii kwa amani na huru wa kashfa hizi za PT ", Patricia Soares, mfanyakazi wa serikali mwenye umri wa miaka 43, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.