MAREKANI-IS-USALAMA

Marekani: IS yapoteza wapiganaji wengi Desemba 2015

Picha ya propaganda iliyorushwa na vyombo vya habari vya kijihadi Welayat Raqa inaonyesha wapiganaji wa kundi la Islamic State wakifanya mazoezi ya kijeshi katika mitaa ya mji wa Raqa, Juni 30, 2015, Syria.
Picha ya propaganda iliyorushwa na vyombo vya habari vya kijihadi Welayat Raqa inaonyesha wapiganaji wa kundi la Islamic State wakifanya mazoezi ya kijeshi katika mitaa ya mji wa Raqa, Juni 30, 2015, Syria. AFP/WELAYAT RAQA/AFP/

Muungano wa kimataifa unaongozwa na Marekani uliwaua wapiganaji 2,500 wa kundi la Islamic State (IS) mwezi Desemba 2015 katika mashambulizi ya anga nchini Syria na Iraq, msemaji wa jeshi la Marekani, Steve Warren, amesema Jumatano hii.

Matangazo ya kibiashara

Pentagon mpaka sasa imekua imejizuia kutoa matokeo ya operesheni hizo. Tangazo la Kanali Steve Warren kwa vyombo vya habari, mjini Baghdad, linakuja wakati ambapo viongozi wa muungano huo wanasisitiza kuhusu kushindwa hivi karibuni kwa kundi la IS.

"Mwezi Desemba, tunakadiria takriban wapiganaji 2,500 waliuawa na mashambulizi ya anga ya muungano wa kimataifa nchini Iraq na Syria", amesema Kanali Warren.

Msemaji huyo wa jeshi la Marekani ameongeza kuwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya anga mwezi Agosti mwaka 2014, kundi la IS lilipoteza hadi kilomita mraba 22 000, sawa na 40% ya maeneo iliyokua ikidhibiti nchini Iraq na kilomita mraba 2,000, sawa na 10%, nchini Syria.

"Tunaamini kwamba IS kwa sasa imeanza kujihami". Kundi hili lilifikia kilele cha shughuli zake mwezi Mei, lakini tangu wakati huo liliendelea kupoteza baadhi ya maeneo lililokua likidhibiti", ameongeza kanali Steve Warren.

Na kama wanajihadi wanaendelea kushindwa nchini Syria na Iraq, wameweza kufanikiwa maeneo mapya mahali pengine, kama vile nchini Libya ambako wanajaribu kuchukua udhibiti wa vituo kadhaa vya mafuta katika bandari mbalimbali.

Mkakati wa muungano wa kimataifa dhidi ya kundi la IS ulikuwa hasa kudhibiti miundombinu ya mafuta inayotumiwa na kundi la kigaidi kwa kujifadhili. Kwa mujibu wa Bw Warren, uzalishaji wa mafuta kutoka kwa maeneo yanayodhibitiwa na kundi la IS umepungua kwa 30%, kutoka mapipa 45,000 hadi 34,000 kwa siku.