VENEZUELA-MVUTANO-SIASA

Venezuela: mgogoro kati ya serikali na upinzani wazua mgogoro wa kitaasisi

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Januari 6, 2015, mjini Caracas.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Januari 6, 2015, mjini Caracas. AFP/PRESIDENCIA/AFP

Siku mbili baada ya upinzani nchini Venezuela kuchukua hatamu ya uongozi wa Bunge, nchi hiyo imejikuta katika mgogoro wa taasisi unaosababishwa na mgongano kati ya serikali ya Nicolas Maduro na upinzani, wakati ambapo nchi hiyo tayari inashuhudia mdororo mkubwa wa kiuchumi.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatano, siku moja baada ya Bunge jipya lililochaguliwa Desemba 6 kushika hatamu ya uongozi, siku ya kwanza ya shughuli za bunge imegeuka kuwa mapambano kati ya Bunge na serikali.

Katika hali ya sintofahamu kwa utawala unaoendelea wa Hugo Chavez (jina la hayati  rais Hugo Chavez), tangu mwaka 1999, muungano wa upinzani, unaotambuliwa kwa jina la MUD, umekwenda kinyume na uamuzi wa Mahakama kuu kwa kuwarejesha kwenye nafasi zao Wabunge watatu wapya wanaopinga sera za Hugo Chavez, ambao walikua walisimamishwa.

Kwa sasa upinzani ukiwa na viti 112 kwa jumla ya 167 katika Bunge nzima la Venezuela, muungano wa upinzani MUD unadai theluthi mbili ya kura ambayo inauruhusu kuitisha kura ya maoni, ambayo inalenga kumtimua madarakani rais Nicolas Maduro kupitia punguzo la muda wa muhula wake.

Upinzani umejipa muda wa "miezi sita" ili uwe umemtimua madarakani rais Maduro kwa njia ya kikatiba.

Lakini rais Nicolas Maduro na Wabunge wake 55 wanapinga harakati hizo za upinzani, wakibaini kwamba ni ukiukwaji wa Katiba. Wamekataa kuwatambua Wabunge hao watatu wapya na wako tayari kukata rufaa mbele ya Mahakama kuu.