Iran yawaachilia huru mabaharia 10 wa Marekani

Mabaharia kumi wa Marekani waliokua wamekamatwa kwa kuingia eneo la bahari la Iran, wameachiliwa huru, runinga ya taifaya Iran imearifu

NI aina hii ya moja ya manowari za Marekani iliyopata hitilafu ya kimitambo , Jumanne, Januari 12, katika bahari ya Ghuba, eno la Iran.
NI aina hii ya moja ya manowari za Marekani iliyopata hitilafu ya kimitambo , Jumanne, Januari 12, katika bahari ya Ghuba, eno la Iran. Zane Ecklun / US NAVY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Mabaharia hao walikamatwa Jumanne wakiwa kwenye boti mbili, baada ya boti moja kupata hitilafu za kimitambo wakati wa mazoezi, Marekani imesema.

Afisa wa Marekani amethibitishia shirika la habari la Reuters kwamba mabaharia hao wameachiliwa huru.

Awali, mkuu wa kikosi cha wanamaji cha Iran, Jenerali Ali Fadavi, alisema uchunguzi ulikuwa umeonyesha hitilafu katika mitambo ya kuelekeza boti zilichangia kwa mabaharia hao wa Marekani kuingia bila kukusudia katika eneo la bahari la Iran.

"Tumethibitisha kwamba kuingia kwa Wamarekani hao maeneo yetu ya bahari hakukuwa uchokozi au kwa kusudi la kupeleleza au masuala husika”, Jenerali Ali Fadavi .

Marekani imekuwa ikiwasiliana na Iran juu ya hatima ya meli mbili za Marekani katika bahari ya Ghuba pamoja na mabaharia wake 10.

Awali Tehran ilithibitisha kuwa mabaharia hao wa Marekani wataweza "haraka" kuendelea na safari yao, alisema afisa mmoja wa Marekani.

"Mapema Jumanne mchana, tumepoteza mawasiliano na meli mbili ndogo za kijeshi ambazo zimekua kisafiri kati ya Kuwait na Bahrain. Tumekuwa na mawasiliano na viongozi wa Iran ambao wametufahamisha kwamba wafanyakazi wetu wako salama", afisa wa Marekani ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliliambia Jumanne hii shirika la habari la Ufaransa AFP, bila hata hivyo kusema nini kilichotokea kwa meli hizo mbili.

"Tumepokea hakikisho kwamba mabaharia wataruhusiwa haraka kuendelea na safari yao", chanzo hicho kiliongeza.

Kwa mujibu wa afisa mwingine wa Marekani, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry aliwasiliana kwenye simu na mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif, baada ya tukio hilo kutokea.