MAREKANI-IOWA-UCHAGUZI

Seneta Ted Cruz ashinda jimbo la Iowa, ampiku Donald Trump na Marco Rubio

Seneta Ted Cruz akizungumza na wafuasi wake mara baadaya kutangazwa mshindi katika jimbo la Iowa
Seneta Ted Cruz akizungumza na wafuasi wake mara baadaya kutangazwa mshindi katika jimbo la Iowa REUTERS/Jim Young

Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani, Ted Cruz usiku wa kuamkia leo amefanikiwa kushinda na kuongoza katika jimbo la Iowa na kumshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu Donald Trump. 

Matangazo ya kibiashara

Mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi kwenye jimbo hilo, Cruz amesema ushindi wake ni ishara tosha kuwa anaelekea katika ikulu ya Marekani, na kwamba ushindi huu ni ushindi wa watu wa kawaida wa Iowa.

Ushindi wa Cruz kwenye jimbo hilo haukutarajiwa hapo awali baada ya kura za maoni kuonesha kuwa bilionea, Donald Trump alikuwa akiongoza akifuatiwa kwa karibu na seneta Marco Rubio.

Kwa matokeo haya sasa ni wazi kuwa ni pigo katika harakati za Trump ambaye alikuwa akiamini kuwa angeshinda kweny jimbo hilo lakini sasa ilibidi apiganie nafasi ya pili kati yake na seneta Rubio.

Bilionea Donald Trump (Kushoto) akiteta katika moja ya mijadala ya televisheni na seneta Ted Cruz aliyeshinda jimbo la Iowa) e Ted Cruz.
Bilionea Donald Trump (Kushoto) akiteta katika moja ya mijadala ya televisheni na seneta Ted Cruz aliyeshinda jimbo la Iowa) e Ted Cruz. REUTERS/Mike Blake

Cruz ameendelea kusema kuwa ushindi wa jimbo la Iowa unatuma ujumbe kwa wagombea wa Republican kuwa rais ajaye wa Marekani hatachaguliwa na vyombo vya habari na kwamba hatachaguliwa na maelekezo ya Washington wala watu wenye ushawishi mkubwa.

Seneta Cruz akasisitiza kuwa rais ajaye atachaguliwa na watu makini na wenye nguvu na kuwa na uzalendo kwa nchi yao.

Seneta Cruz ambaye kampeni zake amejikita katika ngazi ya chini, anatarajiwa kutumia ushindi wa jimbo la Iowa kwa kupata asilimia 27.7, huku mchuano mwingine mkali ukitarajiwa kwenye majimbo ya New Hampshire na South Carolina.