MAREKANI-CUBA-USHIRIKIANO-DIPLOMASIA

Barack Obama kwa vijana wa Cuba: "hatima ya Cuba mikononi mwenu!"

Barack Obama asalimu baada ya hotuba yake katika ukumbi wa Grand Theatre mjini Havana, Machi 22, 2016.
Barack Obama asalimu baada ya hotuba yake katika ukumbi wa Grand Theatre mjini Havana, Machi 22, 2016. NICHOLAS KAMM / AFP

Katika siku ya mwisho ya ziara ya kihistoria, Obama ametetea kwa nguvu zote uhuru wa kujieleza kwa Wacuba wote. bila kubagua.

Matangazo ya kibiashara

Katika hotuba aliyoitoa katika ukumbi Grand Theatre mjini Havana, hotuba ambayo ilirushwa hewani moja kwa moja kwenye runinga ya serikali, Rais wa Marekani amehakikisha kwa mara nyingine tena kwamba hakuja nchini Cuba kulazimisha mabadiliko ya utawala wa Castro.

Hata hivyo Barack Obama anaamini katika mabadiliko ya kisiasa nchini Cuba, ambayo amesema lazima yapitie kwa kizazi cha vijana wa Cuba.

Wakati wa ziara hiyo, Rais wa Marekani pia amezungumzia kuhusu sera ya ndani. Bunge la Congress linakabiliwa na shinikizo, wakati ambapo Wabunge wengi kutoka chama cha Republican wanaendelea kupinga kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Cuba. Kama ilivyotarajiwa rais wa Marekani hakuweza kukutana na Fidel Castro. Hata hivyo alikutana na wapinzani kadhaa wa Cuba, ambapo amewasifu kwa ujasiri wao wa ajabu.

Wakati wa hotuba yake katika ukumbi wa Grand Theatre mjini Havana, iliyochukuliwa kama safari ya kwanza ya rais wa Marekani nchini Cuba kwa miaka 88, Barack Obama aliiomba serikali ya Cuba kutoa uhuru wa kutosha kwa raia wake, huku akibaini kwamba kunahitajika mikakati ya kutosha ili uchaguzi ufanyike katika mazingira bora. Lakini alisisitiza kuhusu jukumu ambalo vijana wa Cuba wanatakiwa kufanya katika mustakabali wa nchi hiyo.